Girumugisha Aibua Vita ya Usajili, Yanga Yafuatilia Kwa Karibu
KIUNGO mshambuliaji wa Al Hilal, Jean Claude Girumugisha, anatajwa kuwa mbioni kuondoka katika klabu hiyo baada ya kupokea ofa nono kutoka klabu ambayo bado haijawekwa wazi.
Taarifa zinaeleza kuwa Girumugisha ni miongoni mwa wachezaji wanaowindwa na Yanga katika dirisha kubwa la usajili, huku mabingwa hao wakitaka kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu wa 2026/27.
Kwa mujibu wa taarifa, uongozi wa Al Hilal unatambua kuwa nyota huyo yuko karibu kuondoka kutokana na uzito wa ofa aliyopokea, ambayo inaelezwa kuwa ni vigumu kuikataa.
Girumugisha amekuwa mmoja wa wachezaji tegemeo wa Al Hilal kutokana na kiwango chake bora, kilichovutia klabu kadhaa barani Afrika, ikiwemo Yanga, ambazo zinaendelea kusaka saini yake kuelekea msimu mpya.
Hata hivyo, hadi sasa bado haijawekwa wazi ni klabu gani iliyowasilisha ofa hiyo wala thamani ya dili hilo, huku taarifa zaidi kuhusu hatma ya kiungo huyo zikitarajiwa kutolewa katika siku zijazo.
Endapo uhamisho huo utakamilika, Girumugisha ataungana na orodha ya nyota wanaoondoka Al Hilal katika dirisha hili la usajili, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kufahamu atatua katika klabu gani.