Yanga SC

Mngqithi Atamka Makubwa Yanga, Aitaka CAF Champions League

Vardo July 11, 2026 12:21 pm

KOCHA Mkuu mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema amejiunga na klabu hiyo akiwa na dhamira ya kuirejesha katika kilele cha soka la Afrika kwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).

Mngqithi amesema amekuwa akiifuatilia Yanga kwa muda mrefu na anaifahamu vyema historia yake, akieleza kuwa ni miongoni mwa klabu kubwa zaidi barani Afrika zenye mashabiki wengi na utamaduni wa ushindani unaoweka matarajio makubwa ya mafanikio.

Mbali na ndoto ya kutwaa taji la Afrika, kocha huyo amewahakikishia mashabiki kuwa Yanga itaingia msimu wa 2026/27 ikiwa na lengo la kutwaa ubingwa wa sita mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuendelea kudumisha ubabe wake kwenye soka la ndani.

Mngqithi pia amesema moja ya malengo yake ni kulirejesha Kombe la Shirikisho la CRDB, ambalo Yanga ilishindwa kulitwaa msimu uliopita, akisisitiza kuwa timu yake itapambana kwenye kila mashindano itakayoshiriki.

Amepongeza uongozi wa klabu kwa kazi kubwa iliyofanyika katika usajili wa wachezaji, akisema umefanikiwa kumpatia kikosi chenye ubora na sifa anazohitaji ili kutekeleza falsafa yake ya mchezo.

Kocha huyo ameema msingi wa mafanikio ya Yanga chini yake utakuwa ni nidhamu, kujituma, mshikamano na uwajibikaji, akieleza kuwa maadili hayo ndiyo yatakayokifanya kikosi kiwe imara ndani na nje ya uwanja.

Kuhusu mfumo wa uchezaji, Mngqithi amesema Yanga itacheza soka la kushambulia, lenye pasi za haraka na presha kubwa kwa wapinzani.

Amefafanua kuwa mara tu timu inapopoteza umiliki wa mpira, wachezaji wake watahitajika kuupokonya haraka iwezekanavyo.

Mngqithi amehitimisha kwa kueleza kuwa ana imani kubwa na kikosi alichokikuta, akisisitiza kuwa kwa ubora wa wachezaji, ushirikiano wa viongozi na sapoti ya mashabiki, Yanga ina kila sababu ya kuwa miongoni mwa timu zitakazoogopwa zaidi barani Afrika.

Kukosa Penalti Janga Kombe La Dunia