Home Uncategorized MORRISON: NINGEPANDA NDEGE INGEKUWA DHARAU KWA WENZANGU…

MORRISON: NINGEPANDA NDEGE INGEKUWA DHARAU KWA WENZANGU…

Na Saleh Ally
Tumezungumza na Bernard Morrison, kiungo mwenye kasi wa Yanga kuhusiana na ule utata wa sauti yake iliyovuja akikubali kupokea fedha za Simba.


Ilisikika akisema kuwa kweli alichukua dola 5,000 (Sh milioni 11.5) kwa mtu aliyemtaja kuwa rais wa Simba na zilipelekwa kwake na wakala. Katika mahojiano yetu yaliyochapichwa na gazeti hili juzi, alieleza ilivyokuwa hadi wakala akampa fedha hizo.


Akaeleza namna alivyoutaarifu uongozi wa Yanga kuhusiana na wakala huyo lakini baadaye akaeleza namna alivyoudhiwa na mmoja wa viongozi anayemuamini kutokana na uamuzi wake wa kusambaza sauti yake hiyo ambaye yeye aliona ni uungwana kumtaarifu kiongozi huyo.


Swali la mwisho ambalo tulimuuliza juzi Jumatano ni kwamba, pamoja na kukubali kupokea fedha zile zilizoelezwa kuwa ni za Simba, je, alizirudisha au la na kama la, matumizi yake yalikuwaje na amebaki na kiasi gani?


SALEHJEMBE: Zile fedha dola 5,000 kutoka kwa wakala, nilisikia zinatakiwa kurudi, umefanyaje? Kama unazo, unaweza kuniambia umetumia kwenye mambo gani?

Morrison: Ndiyo, nimerudisha zile fedha kwa yule ajenti. Nimerudisha fedha kama siku nne zilizopita, maana alisema ninataka kumuingiza matatizoni.


SALEHJEMBE: Kwa hiyo zile fedha alikutumia kutoka Ghana, umezirudisha huko au umefanyaje?
Morrison: Ndiyo, alinitumia kutoka Ghana, nami nimefanya hivyo, nimemrudishia zile fedha.


SALEHJEMBE: Jambo jema, lakini hukwenda Shinyanga kuipigania Yanga, nini tatizo, suala la zile fedha linahusika?
Morrison: Hapana, suala la fedha halipo kabisa hapa. Niwaombe radhi mashabiki kuwa kwa nini sikwenda Shinyanga. Kabla nilikuwa nina maumivu makali katika kidole changu hapa, daktari aliniambia nibaki nyumbani kwa mapumziko ya siku chache.

Nakumbuka siku tatu nne nikiendelea na matibabu hadi tulipokwenda kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya KMC, kama unakumbuka sikucheza.

SALEHJEMBE: Ulikuwa umeshapumzika, au uliona haitoshi?
Morrison: Sikuwa nimefanya mazoezi na siku mbili zilizokuwa zinafuatia ndiyo walikuwa wanasafiri kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo. Kwa mchezaji wa kulipwa, kawaida hauwezi kusafiri na timu kama haujafanya mazoezi na timu.


SALEHJEMBE: Kutokana na hali hiyo uliamua vipi?
Morrison: Niliona ni sahihi kubaki Dar es Salaam, niwasubiri wenzangu wakati nikiwaombea. Ningeungana nao baada ya kurejea. Lakini hawakunielewa kabisa, aliporudi kocha wakasema wataninunulia tiketi ya kwenda Mwanza kwa ndege, halafu Shinyanga.


SALEHJEMBE: Ndege ni rahisi kufika, lakini bado hukwenda na hata kocha Eymael alilalamika?
Morrison: Nilikubali kwenda kweli lakini baada ya kutafakari, nikaona bado haikuwa sawa na lazima kuonyesha nidhamu kwa wachezaji wenzako. Angalia, sikuwa nimefanya mazoezi, vipi niende nikacheze lakini sikuwa nimefanya mazoezi, wenzangu waliofanya mazoezi na wamekwenda na basi, mimi niende na ndege, hii haikuwa sahihi pia na kutowaheshimu wenzangu.


SALEHJEMBE: Sasa baada ya uamuzi huu uliwasiliana na uongozi au kocha?
Morrison: Inawezekana hapa nilikosea lakini nitakuambia kwa nini, sikuwasiliana na mtu. Nikaamua kukaa kimya kwa kuwa mara mbili nawaelewesha hawanielewi, nikaona ni vizuri kuwaheshimu wenzangu (wachezaji) na siku moja nitaeleweka na kwa wengine pia.


SALEHJEMBE: Mtu akikuuliza, sababu hasa ya kutokwenda Shinyanga na baadaye Dodoma ni nini hasa utasema ni heshima kwa wachezaji wenzako tu?
Morrison: Ndiyo hiyo sababu mojawapo lakini kweli mimi nilikuwa majeruhi, wachezaji na viongozi wanajua hili, muulize yeyote, pia si sahihi usafiri na timu kwenda kucheza wakati ukiwa na majeraha.


SALEHJEMBE: Uliona kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na wewe kugoma kwenda, ilielezwa kwamba ni suala la mkataba lilichangia wewe kuweka ugumu?
Morrison: Mimi ni mchezaji ninayejielewa, najua nina mkataba Yanga hadi mwezi ujao, lazima niiheshimu Yanga na ninajua Yanga ni klabu kubwa, siwezi kuivunjia heshima. Lakini kunapokuwa na sababu za msingi na watu wanaziona lazima waniheshimu pia na kweli nilichukizwa hasa na kiongozi ambaye ni msemaji (mhamasishaji) wa klabu yetu.


SALEHJEMBE: Unazungumzia Antonio Nugaz, kipi hasa kilikukwaza?
Morrison: Alikwenda mtaani na kuitangazia jamii kwamba sitaki kwenda Shinyanga, alionyesha sipatikani kwenye simu na akapiga simu hata mbele za watu kuwa simu yangu imezimwa. Kwangu hii ni kukosa weledi kabisa, vipi uwaonyeshe watu Tanzania nzima mimi eti sipatikani. Yeye anafanya kazi Yanga, mimi pia, na Yanga ni brand kubwa sana, vipi mambo ya ndani kama yale uweze kusema hadharani vile.
Mimi nilidhani anaweza kumlinda mchezaji mbele ya jamii, kuilinda nembo ya Yanga na kama kuna kosa mnamalizana ndani kama wafanyakazi wa klabu.


SALEHJEMBE: Ulipenda akulinde?
Morrison: Kama kweli ningekuwa nimefanya kosa, bado alistahili kunilinda, lakini sikuwa na kosa na bado hakupaswa kufanya alichokifanya kwa ajili ya heshima ya klabu yetu.


SALEHJEMBE: Ulipata nafasi ya kuzungumza na kumueleza kilichokukwaza ili muwe sawa na kufanya kazi kwa furaha huko mbele?
Morrison: Sina tatizo naye, ila mimi ni mkimya, sipendi sana kuzungumza. Hivyo, sijamfuata na wala sitamfuata kwa ajili ya hili suala, najua Nugaz si mtoto, ni mtu mzima, atakuwa anaelewa. Jiulize, vipi kama anaweza kuipigania klabu halafu hampiganii mchezaji wa Yanga? Naendelea kusisitiza nilikuwa majeruhi na sikuwa fiti ndiyo maana sikusafiri na timu.


SALEHJEMBE: Wakati mwingine ni vizuri kuzungumza mkaweka mambo sawa baada ya kutokea hali fulani ya sintofahamu baina yenu?
Morrison: Ni kweli lakini mimi niko tofauti kidogo, ninacholenga zaidi hapa ni kile kilichonileta Tanzania, najua nipo hapa kucheza soka na kuisaidia timu ninayoitumikia, ndiyo maana siwezi kumuuliza Injinia Hersi kuhusiana na kusambaa kwa sauti ya mawasiliano yetu wala siwezi kumuuliza Nugaz alivyonifanyia mbele ya vyombo vya habari na kunichongea kwa mashabiki.


SALEHJEMBE: Umerudi uwanjani, hii ni baada ya haya mambo mengi ya mapito na mkataba wako unaelezwa ni miaka miwili sasa, wewe leo umesema ni miezi sita, unaisha mwezi ujao. Unabaki Yanga, unaondoka au nini umepanga maana hadi sasa haujaongeza mkabata?

Morrison: Kwenye hili ningependa kuwa wazi sana……..


MALIZIA SEHEMU YA MWISHO….

SOMA NA HII  YANGA WAPATA MTEREMKO KOMBE LA SHIRIKISHO, SINGIDA UNITED MAJANGA