NA SALEH ALLY
TIMU ya Yanga ni kati ya zile kubwa na kongwe zaidi hapa nchini.
Hii ni kati ya timu zile za mwanzoni kabisa kwenye historia ya soka hapa nchini na imefanikiwa kuufanyia kazi ukongwe wake kwa kuwa ndiyo kinara wa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hii ni sifa ambayo huwezi kuiondoa kwao, labda iibuke timu nyingine na kuwapiku ingawa linaonekana kuwa ni jambo ambalo linaweza kuchukua muda kidogo.
Ni timu ambayo inatajwa kuwa na mashabiki wengi zaidi hapa nchini, wenyewe wanaiita timu ya wananchi, lakini kwa misimu mitatu sasa, Yanga hii imeshindwa kufanya mambo makubwa ambayo yamekuwa yakisubiriwa na mamilioni ya mashabiki wao.
Huu ni msimu wa tatu, Yanga wanaukosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kibaya zaidi ni kwamba mara zote ubingwa huo unakwenda kwa watani wao wa jadi Simba.
Hili limekuwa jambo ambalo linawaumiza sana mashabiki hao wa Jangwani, lakini hawana la kufanya kwa kuwa soka siku zote lazima liwe na mshindi, hata kama mtafanyaje lazima mwishoni mshindi atapatikana.
Asilimia zaidi ya 100 ya timu zote ambazo zimefanikiwa kutwaa ubingwa kwenye ligi zao, zimefanya hivyo kutokana na maandalizi mazuri kuwazidi wapinzani wao.
Hili halina ubishi, ili Yanga watwae ubingwa wanatakiwa kuwa na maandalizi bora zaidi ya timu nyingine 19 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, jambo ambalo wamelikosa kwenye miaka yote mitatu mfululizo.
Kwa msimu huu ni dhahiri kuwa Yanga sasa wanapambana kuhakikisha kuwa wanamaliza kwenye nafasi ya pili kwenye ligi, lakini pia wakiwa na nafasi ya kuchukua ubingwa wa FA ambao kama wakifanikiwa basi utawapa nafasi ya moja kwa moja ya kwenda kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambalo ni la pili baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo watashiriki Simba.
Pamoja na kwamba Yanga wameonekana kupambana sana, lakini msimu huu wanatakiwa kuchukua funzo moja kubwa sana, kuwa walishindwa kufanya maandalizi mazuri kwenye suala la usajili.
Yanga wanaweza kuwa wametua fedha nyingi zaidi kwa ajili ya usajili msimu huu kuliko misimu miwili au mitatu iliyopita, lakini walisajili ovyo na bila kufuata utaalamu.
Au wakati mwingine unaweza kusema kuwa Yanga walikuwa na pupa na hawakutaka kuwa na subira ambayo labda mwishoni ingewapa matunda waliyokuwa wanayategemea.
Kumbuka kuwa mwanzoni mwa msimu Yanga walitajwa kuwa timu ambayo ilifanya usajili wa wachezaji wengi sana, walisajili wachezaji waliokuwa wamewika kwenye timu zao kama Juma Balinya, Sudney Urkhob, Maybin Kalengo, Issa Bigirimana Patrick Sibomana, David Molinga na Tariq Seif. Wengine ni Metacha Mnata, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama na wengine wengi.
Lakini kumbuka kuwa asilimia kubwa ya wachezaji hao walidumu Yanga kwa miezi isyozidi mitatu tu na mwisho wakawaacha, wakiwemo Juma Balinya, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo na Issa Bigirimana kwa kile walichodai kuwa wanataka kuboresha kikosi chao na hao hawana kiwango.
Hata Yanga waliposajili tena walionekana kuwa na pupa kama za mwanzoni, ndiyo maana pia wakajikuta wakimsajili mshambuliaji Ditram Nchimbi wakiamini kuwa atakuwa bora zaidi kwao na kuwapa ubingwa kwa kuwa tu aliwafunga mabao matatu kwenye sare ya 3-3 dhidi ya Polisi Tanzania.
Lakini pia wakawasajili wachezaji kama Adeyum Saleh na Tariq Seif ambao nao hawajawapa kile ambacho walikuwa wanakitarajia.
Hili linatakiwa kuwa funzo kubwa kwao wakati wanajiandaa na msimu ujao na kama watapata nafasi ya michuano ya kimataifa kuwa wanatakiwa kuwa watulivu na kutafuta wataalam sahihi ambao wanaweza kuwasaidia kwenye kufanya usajili badala ya kufanya pupa ambazo mwisho wake haziwezi kuwapa matunda.
Ukitazama Yanga ya leo inawika na mastaa wale wale ambao awali walionekana kuwa siyo bora kwa kuvaa jezi ya Jangwani kama Deus Kaseke, Mrisho Ngassa, Juma Abdul na Kevin Yondani.