KAMPUNI ya Burudani na Michezo, SportPesa Limited jana imewakabidhi Mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/2020, Simba hundi ya milioni 100 huku Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Haji Manara akitamba bado wanahitaji mawili ili wafikishe matano mfululizo.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika kwenye Ofisi za SportPesa zilizokuwepo Peninsula House, Masaki jijini Dar es Salaam iliyohudhuriwa na viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo.
Simba wikiendi iliyopita ilitwaa ubingwa huo baada ya kutoka suluhu na Tanzania Prisons mchezo uliopigwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya ikifikisha pointi 79 katika msimamo wa ligi.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas alianza kwa kuwapongeza wachezaji na viongozi kwa kufanikiwa kuchukua ubingwa.
“Awali ya yote nianze kwa kuwapongeza viongozi na wachezaji wa Simba, kwani mmewapa heshima kubwa Wanamsimbazi kote nchini na kubwa zaidi ni heshima mliyotupa sisi kama wadhamini wenu wakuu kwa mafanikio makubwa katika kipindi chote cha miaka mitatu.
“Simba imetendea haki nembo yetu ya SportPesa na kama kampuni inaamini sisi kuwa wadhamini wakuu imekuwa ni moja ya chachu iliyosababisha Simba kuchukua ubingwa huu.
“Tunachokifanya leo (jana) ni kutimiza moja ya ahadi yetu tuliyoitoa wakati tunasaini mkataba wa udhamini mwaka 2017 kuwa tutatoa bonasi ya Sh 100 Mil endapo mojawapo ya timu tunazozidhamini itachukua ubingwa wa ligi, hivyo bila shaka timu ni Simba imechukua ubingwa huo,”alisema Abbasi.
Akitoa shukrani hizo, Manara alisema kuwa “Tunawahaidi wadhamini wetu wa Simba ambao ni SportPesa kuendelea kuwa tumepanga kuchukua ubingwa wa ligi kwa mara tano mfululizo, hivyo tumebakisha makombe mawili ya ligi tufikishe malengo yetu.