NA SALEH ALLY
NILIKUWA nikiiangalia kwenye runinga mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports kati ya Azam FC waliokuwa wakiwavaa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba.
Kawaida, Simba na Azam FC zinapokutana inakuwa ni ‘open game’ na zinacheza kwa kujiachia sana. Hivyo kuufanya mpira kuwa na mashambulizi mengi sana mfululizo.
Mechi ya juzi kwenye Uwanja wa Taifa ilikuwa nzuri sana lakini niliona kama dakika za mwisho, mambo yalibadilika na ikawa si kama wengi walivyotarajia.
Azam FC walipoteana na kuwapa Simba nafasi ya kucheza muda mwingi mpira wanavyotaka wenyewe. Pasi za dharau na mbwembwe, manyanyaso waliyoanza kupata Azam FC, unaweza kuifananisha na timu ya kawaida sana.
Wakati mwingine inafikia unaanza kuona kama Azam FC haikustahili kufika robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu kutokana na ilivyoonekana ni dhaifu sana kwa Simba ambayo ilikuwa katika kiwango chake bora ikifanya inavyotaka bila ya woga.
Najua hili kwa viongozi wa Azam FC watakuwa wameliona na kulifanyia kazi na hili mimi nilikuwa ninapita tu kwa kuwa ninachotaka kukigusa ni kile kilichofanywa na kiungo wa Azam FC, Frank Domayo.
Domayo ambaye ni kiungo wa zamani wa Yanga, alimrukia na kumkaganya vibaya mguuni beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe ambaye aliumia sana na kujawa na hasira hali iliyosababisha atake kuzichapa na Domayo lakini wenzake wakamzuia.
Nimesikia Domayo akisema alitaka kumuomba msamaha lakini akaona alitaka kumvamia na kumpiga, akaamua kuondoka na kuingia vyumbani.
Hili bado haliwezi kuwa suluhisho kwa Domayo kutokana na alichokifanya. Kwanza ni kosa lakini inafikirisha kwamba vipi anaweza kuamua kumrukia kijana mwenzake hali inayoonyesha wazi alitaka kumuumiza.
Ukiangalia vizuri, kabla ya kumrukia Kapombe katika dakika ya 90, Domayo alifanya matukio hayo kama mara mbili hivi, mara moja ikiwa dhidi ya Clatous Chama ambaye alimkwepa.
MOJA:
Lazima Domayo anajua Kapombe amekuwa akisumbuka na majeraha kwa muda mrefu hadi alipopata nafuu na kucheza.
MBILI:
Domayo anajua ugumu wa maumivu yanayomuweka mchezaji nje na mateso yake kwa kuwa mara kadhaa amekuwa majeruhi na kulazimika kukaa nje.
TATU:
Bila ubishi Domayo anajua ugumu wa kutibu majereha na wakati mwingine kulazimika kusafiri nje ya nchi mara kadhaa.
NNE:
Lazima Domayo anajua gharama kubwa inayotokana na majeraha, klabu inaweza kuhudumia lakini kuna wakati mchezaji analazimika kutoa chake.
TANO:
Haina ubishi Domayo anajua, yeye na Kapombe ni watu wa umri unaofanana, wanapigania maisha, uzima wao ndio ubora wa maisha yao. Maumivu ya majeraha ni maumivu ya moyo na akili.
Sijajua siku hiyo alikuwa wapi kiakili, sijui kipi kilimkwaza au kumkasirisha kwa kiasi kile. Hakika ni kitu kinachoumiza kwa wanaofikiria, kinachofikirisha kwa wanaoweza kutaka kujua zaidi.
Binafsi, bado naweza kusema Domayo anaweza kusamehewa kwa ajili ya kosa alilofanya ili ajifunze zaidi. Tukubali ndani ya uwanja kuna “shetani” wake lakini lazima wahusika wanaocheza wajue namna ya kumdhibiti.
Kwangu naona Domayo kwa walivyo na Kapombe, simu haitoshi, anaweza kumtafuta na kumpa pole ana kwa ana. Safari hii hawezi kuwa na zile hasira za uwanjani kama juzi.
Bado Domayo ana nafasi ya kujirekebisha na baada ya hapa tutaona kama suala hili lilimuumiza kweli na alilijutia kwa kuwa kama uzima upo, tutaendelea kumshuhudia ingawa kabla ya kutenda jambo, vizuri kutafakari mambo mengi ya muhimu hasa kama inahusiana na maisha ya wenzako pia.