Home Uncategorized HII HAPA, HADITHI YA YANGA NA MABAO 36 YA WAZALENDO….

HII HAPA, HADITHI YA YANGA NA MABAO 36 YA WAZALENDO….


Na Saleh Ally
KINARA wa kufunga mabao katika kikosi cha Yanga ni David Molinga Ndama maarufu kama Falcao ambaye ametikisa nyavu mara 10.


Raia huyu wa DR Congo amekuwa gumzo baada ya mara kadhaa kugeuka shujaa baada ya mashabiki kumzomea lakini baada ya kufunga mara ya mwisho katika Kombe la Shirikisho, Yanga ikiivaa Kagera Sugar, inaonekana sasa mambo yamekaa poa.


Hakuna ubishi, msimu huu wa 2019-10, licha ya kuwa Yanga inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiendelea kuipambania nafasi hiyo kwa kuwa tayari mabingwa, Simba wameshatangazwa lakini suala la safu yake ya ushambulizi, linabaki kuwa mjadala.


Mjadala huo ni hivi; Yanga haikuwa katika zile timu zilizofanya vizuri katika ufungaji. Unaweza kusema haikuwa na safu kiwembe ya ushambulizi kama ambavyo ungetegemea kuona safu ya ushambulizi ya Yanga inachuana vikali na yeyote anayeonekana mkali kama ilivyo vinara Simba.


Unaona katika mechi 32 za Ligi Kuu Bara, Yanga imefunga mabao 38, Simba katika mechi hizo 32 imefunga mabao 69, ukigawa mara mbili unapata 34.5, yaani ni zaidi ya mara mbili ya yale ambayo wamefunga Yanga. Hili ni jambo la Kisayansi na linapaswa kupewa nafasi kwa kuwa ukweli wake ni hesabu na ziko wazi kwamba Yanga hawana fowadi nzuri msimu huu na wanapaswa kuifanyia kazi.


Wakati wanatafakari hilo, hapa kuna jambo la kujifunza na lengo si kuwalaumu Yanga lakini kuangalia kadhaa ambayo maswali yake yanaweza kutumiwa kutafakari mambo kadhaa.

MHILU…

Najadili kwa upande wa klabu yenyewe ya Yanga lakini upande wa wachezaji pia. Angalia, safu ya wafungaji bora inaongozwa na mchezaji wa kigeni, Meddy Kagere wa Simba, raia huyu wa Rwanda ana mabao 19 kileleni mwa ligi hiyo akiwa anafuatiwa na mlolongo wa wazalendo.


Anayemfuatia ni Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar mwenye mabao 13, halafu Realiant Lusajo wa Namungo FC, mwenye mabao 12, Paul Nonga wa Lipuli ana 11, Peter Mapunda wa Mbeya City ana mabao 10 sawa na Daruwesh Saliboko wa Lipuli FC. Wageni wenye mabao 10 ni Molinga na Bigirimana Blaise wa Namungo FC.


Ukiangalia vizuri wachezaji wenyeji au wazalendo wanaomfukuza Kagere wenye mabao 13, 12 na 11 wote walikuwa wachezaji wa Yanga na wakashindwa kufanya vizuri kama wanavyofanya sasa.


Ukijumlisha mabao yote hayo waliyofunga, maana yake kwa sasa wana jumla ya mabao 36 ya Ligi Kuu Bara ambayo ni takribani yale ambayo wamefunga Yanga kwa msimu wote hadi sasa.

Ukipiga hesabu utaona hivi, wazalendo hawa wote watatu, kila mmoja ana mabao mengi kuliko mfungaji bora wa Yanga, yaani Molinga aliyefunga 10 ambaye ni raia wa kigeni na ninaamini analipwa mshahara mkubwa zaidi yao.

Tujifunze, kama Mhilu ambaye ni kiungo wa pembeni anaweza kufunga mabao mengi  kuliko mchezaji yeyote Yanga, vipi alishindwa kufanya hivyo akiwa Yanga?


Hali kadhalika, angalia kwa Nonga na Lusajo ambaye alionekana hawezi kabisa. Jambo la kujifunza hapa, nikianza na wachezaji, kwamba wana kila sababu ya kutulia na kujiamini.

 LUSAJO…

Yanga ni timu kubwa kweli, presha yake inakuwa juu ukilinganisha na timu nyingine, ukiachana na Simba. Lakini kwa kuwa kazi yao inakuwa ni kufunga na kuisaidia timu, lazima wajiamini na kufanya kazi yao kwa ufasaha.


Sehemu ya ubora wa mchezaji ni kuonyesha kiwango bora hata wakati wa kipindi cha presha kubwa.


Kwa klabu au hizi timu kubwa, mara nyingi tumeona zikiwavumilia wachezaji wa kigeni na kuwapa nafasi wazoee mazingira. Hili halifanyiki hivyo kwa wachezaji wazalendo na kuna kitabia cha kuwadharau wachezaji wa nyumbani.

NONGA AKIWA YANGA…

Shida hii, mara nyingi hujengwa na mashabiki ambao wanaangalia mambo kishabiki na hiyo ni haki yao lakini unakosa kiongozi mwenye msimamo, anayejiamini na kutambua mambo anayeweza kusema Mhilu ni bora au Lusajo ni mzuri lakini anahitaji muda na sisi tutaendelea kubaki naye.


Kiongozi akishapigiwa kelele tu, anaingia uoga na mara moja anataka mchezaji aachwe. Msimu mmoja au miwili, anakuwa tishio akiwa na timu nyingine, Hili linakuwa ni tatizo la kutokuwa na subira hata kidogo au kuona mbele lakini ni kukosa misimamo kwa viongozi wa klabu ambao wanakuwa wanapelekeshwa na mashabiki na kupoteza maana ya kuwepo kwa viongozi.



TOP 5, WAFUNGAJI WAZALENDO:

1.   Yusuf Mhilu-13 (KageraSugar)
2.   Realint Lusajo-12 (Namungo FC)
3.   Paul Nonga-11 (Lipuli FC)
4.   Peter Mapunda-10 (Mbeya City)
5.   Daruwesh Saliboko-10 (Lipuli FC)



SOMA NA HII  AZAM FC KUHAMISHIA HASIRA ZA PRISONS KWA KMC