SELEMAN Matola, Kocha Msaidizi wa Simba amesema kuwa watatutumia nguvu kubwa sana kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho hatua ya fainali mbele ya Namungo, inayotarajiwa kuchezwa Agosti 2,kutokana na Uwanja kutokuwa na ubora wa kisasa.
Simba itakutana na Namungo FC kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa Uwanja wa Nelson Mandela uliopo Sumbawanga.
Akizungumza na Saleh Jembe, Matola amesema kuwa ingependeza zaidi iwapo waandaaji wa Kombe la Shirikisho wangechagua uwanja mmoja maalumu kwa ajili ya kombe hilo ambalo lina heshima tofauti na kuupeleka kila mkoa.
“Waandaaji wamefanya jambo zuri kupeleka mchezo nje ya Dar es Salaam lakini wanapaswa waangalie kwamba kuna mazingira ambayo yatakuwa si rafiki kwa wachezaji hasa kwenye mchezo mkubwa kama fainali kupelekwa Sumbawanga kwenye uwanja ambao unaanza kufanyiwa marekebisho kwa sasa.
“Ninadhani itakuwa fainali ngumu na wachezaji hawatatoa burudani ile ambayo imezoeleka kama ingekuwa pale Uwanja wa Taifa, hivyo wakati mwingine ningependa kuwashauri hawa waandaaji wawe na sehemu maalumu ya kuchezea fainali ya mashindano haya makubwa, wachague tu hata taifa pale ujue mchezaji kucheza ni CV,” amesema Matola.
Simba ilitinga hatua hiyo kwa kushinda mabao 4-1 mbele ya Yanga Uwanja wa Taifa, huku Namungo ikiibukia fainali baada ya kushinda mbele ya Sahare All Stars bao 1-0 Uwanja wa Mkwakwani Tanga.