Home Uncategorized HII KASI YA LALA SALAMA INGEANZA MWANZO INGEPENDEZA, AZAM FC SIJUI TATIZO...

HII KASI YA LALA SALAMA INGEANZA MWANZO INGEPENDEZA, AZAM FC SIJUI TATIZO LIPO WAPI


NGUMU kuamini unapopokea taarifa ngumu hasa kwenye wakati mgumu kuwa yale mambo uliyokuwa ukihitaji kuyafanya yote yamevurugikavurugika lazima kichwa kipasuke kwa kuwa hukujiandaa kupata taarifa hizo.
Labda inaweza kuwa ni hesabu za Singida United kwa sasa namna ambavyo wanayapokea matokeo magumu kwamba msimu ujao wa 2020/21 watakuwa wakishiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Kinachowaongezea ugumu ni namna jamaa zao walioachana nao msimu uliopita wa 2018/19, Stand United ambao walishuka daraja  inawashuhudia hao wanaibukia Ligi Daraja la Pili, ngumu kuamini lakini ndio taarifa ambazo wanakutana nazo kwa sasa.
Labda ilikuwa ni mipango yao kutokuwa kwenye ramani mwanzoni mwa msimu hasa kwenye upande wa masuala ya kiuchumi pamoja na sapoti kutoka kwa wadau kuna funzo ambalo wanaliacha kwa timu ambazo zimepanda kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Gwambina FC ambao wao wanatoka kundi B pamoja na mabingwa wa jumla wa Ligi Daraja la Kwanza, Dodoma FC wana jambo hapa la kujifunza.
Wakati wao wanapanda njiani wanapishana na timu nyingine ambazo zilikuwa zinaishi ndani ya nafasi ambazo wao wanazitwaa kwa sasa hivyo kwa kuwa wanazipokea basi wana kazi ya kujiandaa pia kuziacha iwapo watajisahau.
Mtifuano wa lala salama ni wa ajabu kwa sasa kwani wakati mwingine unajiuliza hivi hizi timu zama zile zilikuwa wapi kupambania kombe ili kuleta ushindani?
Mpaka Simba inatwaa ubingwa ikiwa na michezo sita mkononi bado walikuwa hawajashtuka kwamba kila timu ina uwezo wa kushinda kwenye mechi ngumu na zile ambazo wao wanazichukulia katika hali ya kawaida.
Imekuwa ni rahisi sana kwa timu za chini kupata matokeo mazuri mbele ya timu kongwe ila zinaboronga pale ambapo zinakutana na timu nyingine ambazo zipo chini ya tatu bora.
Tazama namna Mbao FC na Mwadui zilivyoinyoosha Simba ndani ya ligi, kwa mfano sasa ile kasi ya Mwadui FC wakati inamenyana na Simba ingeendelea palepale mpaka sasa ninaamini wangekuwa ndani ya 10 bora ila leo wanahaha kusaka tiketi ya kubaki ndani ya ligi.
Mbao FC mambo bado magumu kwani baada ya kumpata Kocha Mkuu, Felix Minziro mambo yanakwenda na bado wanamatumaini ya kubaki kwenye ligi licha ya kuwa nafasi ya 17 na pointi 42 wana mchezo mmoja mkononi.
Wameleta ushindani na kuweza kuipa tabu Namungo FC ambayo imeweza kuwanyoosha mabao 3-0 jambo ambalo limeonyesha uhai kwao.
Azam FC sijajua tatizo lao lipo wapi bado ninajaribu kutazama kwa umakini sioni ambapo ninaweza kusema kuna tatizo kwa kuwa ina uwezo wa kupata wachezaji bora hata wale ambao ipo nao kwa sasa ni bora na wana uwezo mkubwa.
Singida United juhudi zenu za kuitungua Ruvu Shooting mabao 2-0 tumeziona hivyo ninawatakia kila la kheri huko Ligi Daraja la Kwanza, moto mliotoka nao huku ndani ya ligi uendelezwe daima na milele.
SOMA NA HII  WINGA AS VITA AKUBALI KUTUA YANGA