KUANZIA wiki jayo, Kamati ya Mashindano ya Yanga ikiwa sambamba na wadhamini wao GSM, inatarajia kuanza kuandaa mapokezi ya kutua kwa kiungo mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Sogne Yacouba.
Taarifa za ndani ya Klabu ya Yanga zimeweka wazi kuwa muda wowote ndani ya wiki ijayo wataanza kupokea wachezaji wao wapya wakianza na Yacouba ambaye yupo huru, baada ya mkataba wake na timu ya Asante Kotoko ya Ghana kumalizika Aprili 2020.
Habari zinaeleza Yacouba, alianza kuviziwa na Yanga, tangu msimu uliopita baada ya aliyekuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kuwasilisha jina lake kwa mabosi hao lakini walishindwa kumpata kufuatia kuwepo kwenye mkataba wa zaidi ya mwaka mmoja na Asante Kotoko.
“Naomba nikupe siri ambayo huijui, siyo kwamba viongozi wetu wamelala, hivyo mnavyofikiria kwenye suala la usajili, ila msichokijua ni kwamba, baada ya msimu huu kumalizika mtamuona yule rasta wa Asante Kotoko, Yacouba akitua hapa maana wameshamalizana naye kwa asilimia 90.
“Huyu jamaa kama hufahamu ni kwamba aliwahi kuwasumbua sana Simba siku ile walipocheza kwenye ule mchezo wao wa Simba Day, mwaka juzi na tangu siku hiyo sisi tulianza kumfuatilia ila tukakwama kumnasa maana alikuwa na mkataba na timu yake.
“Habari njema kwa mwaka huu ni kwamba tayari mkataba wa mchezaji huyo na Klabu ya Asante Kotoko umeisha na kizuri zaidi Kampuni ya GSM wameshafanya yao kwa asilimia nyingi kama nilivyokwambia na bila shaka wiki ijayo baada ya ligi tu kukamilika nadhani utamuona akitua kusaini kwetu.”
Kwa sasa Yanga imekuwa na tatizo katika safu ya ushambuliaji wake, David Molinga ndiye kinara wao wa mabao katika Ligi Kuu Bara akiwa nayo 10 akiwa amezidiwa mabao 12 na straika wa Simba, Meddie Kagere ambaye ni kinara wa ufungaji katika ligi.
Rekodi za jumla katika ligi kuu msimu huu zinaonyesha kuwa Yanga pia imekuwa na idadi ndogo ya mabao ya kufunga tofauti na wapinzani wake wengi wanaoshika nafasi za juu kwenye ligi hiyo.