LIGI Kuu Tanzania Bara, Julai 26 ilishuhudiwa mechi 10 za mwisho za kumalizia msimu wa 2019/20 huku vita ya ubingwa kazi ikiwa imeshaisha baada ya Simba kutwaa ubingwa.
Simba wameliweka jumlajumla kabatini baada ya kubeba kwa misimu mitatu mfululizo walianza msimu wa 2017/18 kisha 2018/19 na 2019/20.
Vita ilibaki kwenye timu ambazo zitashuka daraja pamoja na zile ambazo zitacheza play offs,zilizoshuka daraja ni Alliance FC, Lipuli FC, Ndanda na Singida United.
Zile zitakazocheza playoffs ni Mbao FC v Ihefu na Mbeya City v Ihefu Julai 29 ambayo ni kesho.
Kulikuwa na matukio mengi ndani ya uwanja kwa wachezaji kusaka pointi tatu hapa tunakuletea kikosi cha wachezaji waliokuwa watukutu ndani ya uwanja namna hii.
John Mwenda
Kipa wa Alliance FC alifanya utukutu wake kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City, Uwanja wa Nyamagana. Alimchezea rafu George Chota na alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 71.
Nafasi yake ilichukuliwa na mchezaji wa ndani Siraj Adam. Uongozi wa Alliance ulimpiga panga la shilingi 200,000 kutoka kwenye mshahara wake. Dakika 90 zilikamilika kwa timu zote sare ya bila kufungana.
Israel Patrick Mwenda
Nahodha wa Alliance FC, ilikuwa ni Uwanja wa Nyamagana, Oktoba 31, alimchezea rafu Idd Gomba wa Mbeya City alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 54.
Alipigwa faini ya Sh 250,000 kutoka kwenye mshahara wake.
Lamine Moro
Juni 17, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, Moro wa Yanga alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 88 baada ya kuonyesha ubabe kwa kumchezea rafu nyota wa JKT Tanzania, Mwinyi Kazimoto.
Kazimoto ambaye ni nahodha wa JKT Tanzania naye pia alionyeshwa kadi nyekundu kwa kile kilichoelezwa kuwa alikuwa ni chanzo cha vurugu.
Ally Mtoni ‘Sonso’
Beki huyu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa Januari 18 Uwanja wa Taifa, alimfanyia undava beki wa Azam FC, Nicholas Wadada Uwanja wa Taifa wakati Yanga ikipoteza kwa kufungwa bao 1-0.
Dakika ya 80 alifanya kitendo hicho na bao la ushindi kwa Azam FC alijifunga Sonso katika harakati za kuokoa.
Nicolas Wadada
Beki huyu wa Azam FC kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Januari 18 Uwanja wa Taifa, alimliza Ally Mtoni ‘Sonso’ kimyakimya jambo ambalo halikuonwa na mwamuzi ila kosa la Sonso ilikuwa kulipa kisasi alikutana na kadi nyekundu.
Zawadi Mauya
Zawadi Mauya kiungo wa Kagera Sugar, Septemba 26, Uwanja wa Kaitaba alimchezea rafu Ibrahim Ajibu kwa kumpiga mateke zaidi ya mawili mguuni. Alionyeshwa kadi ya njano. Baadaye alijutia kosa hilo na kuomba msamaha. Kagera Sugar ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0.
Abeid Shamte
Nyota huyu wa Namungo FC alimpiga kiwiko beki wa Simba, Haruna Shamte kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Majaliwa dakika ya 43. Mchezo huo ulikamilika kwa sare ya bila kufungana ilikuwa ni Julai 8, alionyeshwa kadi ya njano.
Pascal Wawa
Januari 4, alimkanyanga nyota wa Yanga, Ditram Nchimbi Uwanja wa Taifa kwenye sare ya kufungana mabao 2-2.
Ishu ilipita kama upepo vile na janga la Corona likafanya majarada yakasukumwa mbali kabisa.
Jonas Mkude
Mkude alimpiga kiwiko mchezaji wa Biashara United, Februari 22 Uwanja wa Taifa, Ally Kombo dakika ya 54 wakati akiuumiliki mpira kisha maisha yakaendelea kwa kuwa mwamuzi hakuliona tukio.
Mkude alikutana na panga la Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kufungiwa michezo miwili pamoja na adhabu ya laki tano.
Bernard Morrison
Mchezaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma alikutana na kiwiko cha Morrison, Februari 15 Uwanja wa Taifa kwenye sare ya bila kufungana. Ishu iliamuliwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kumfungia mechi mbili na faini ya laki tano.
Clatous Chama
Machi 8 Uwanja wa Taifa alimchezea rafu Feisal Salum wa Yanga kwenye kichapo cha bao 1-0 ambacho Simba ilipokea kutoka kwa Yanga. Chama aliomba msamaha kwa mashabiki na Fei Toto.