Home Uncategorized UTEKELEZAJI WA KUBADILI JINA LA UWANJA WA TAIFA WAANZA KWA VITENDO

UTEKELEZAJI WA KUBADILI JINA LA UWANJA WA TAIFA WAANZA KWA VITENDO

WIZARA  ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo imeanza kutekeleza maelekezo ya Rais  John Magufuli wa kubadili jina la Uwanja wa Taifa na kuwa Mkapa Stadium katika kumuenzi Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Wiliam Mkapa.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Michezo wa Wizara hiyo, Yusufu Singo, imeeleza kuwa mchakato umeshaanza na wameshaliondoa jina la zamani ili kuweka jina la Mkapa, kwa maelekezo ya Waziri wa Michezo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

“Baada ya maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli kutaka uwanja huu ubadilike ili tuweze kumuenzi Rais wa awamu ya Tatu, Hayati Benjamini Mkapa, tayari Waziri mwenye dhamana ya michezo na katibu Mkuu wa Wizara ya michezo, wameelekeza tuanze shughuli hiyo mara moja na tumeanza kuliondoa jina la zamani la ‘National Stadium,” alisema Singo.
Singo ameongeza kuwa baada ya kuliondoa jina la zamani la uwanja huo, kuna changamoto kidogo ya kuliweka jina jipya hivyo wanasubiri kukutana na wataalam wa wizara, huku mafundi wakiwa tayari wanaendelea na ujenzi kwenye eneo husika.
Rais Magufuli alitoa maelekezo ya kubadili jina la uwanja wa Taifa, uitwe Uwanja wa Mkapa (Mkapa Stadium), wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye kuuaga mwili wa  MkapaJumanne hii kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
SOMA NA HII  YANGA YAPANIA KUIFANYA SIKU YA WANANCHI YA KIPEKEE ZAIDI