KLABU ya Arsenal usiku wa kuamkia leo imesherehekea taji lake la 14 la Kombe la FA baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Chelsea uliochezwa Uwanja wa Wembley.
Mabao yote mawili ya ushindi yalifungwa na Pierre-Emerick Aubameyang ambaye ni nahodha wa kikosi hicho aliyefunga bao la kwanza dakika ya 28 kwa penalti na dakika ya 67 ambalo lilikuwa la ushindi kwa timu hiyo.
Chelsea ilikuwa ya kwanza kupachika kupitia kwa Christian Pulisic dakika ya 5 ila halikudumu mpaka dakika 90 kwani walipoteza mbele ya Arsenal waliokuwa na kasi ya kusaka ushindi mwanzo mwisho.
Wakiwa kwenye chumba cha kubadilishia nguo wachezaji wa Arsenal walikuwa na shangwe za kutosha kwa kutimiza malengo yao ya kutwaa taji hilo ambalo kwao ni heshima.
Ushindi huo unawapa nafasi ya kushiriki mashindano ya Europa jambo ambalo limemfanya Kocha Mkuu, Mikel Arteta awe mwingi wa furaha kupata mafanikio ndani ya timu hiyo baada ya kuachiwa mikoba na Unai Emery.
Mateo Kovacic wa Chelsea alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 73 na kuwafanya Chelsea wamalize wakiwa pungufu.