Manchester United hatimaye imemalizana na Alexis Sanchez baada ya klabu ya Inter Milan kukubali kumsajili nyota huyo raia wa Chile moja kwa moja, kwa mujibu wa ripoti kutoka nchini Italia.
Kwa mujibu wa gazeti la Corriere della Sera la Italia, limeripoti kuwa Mkurugenzi wa michezo wa Inter Milan, Beppe Marotta amekubaliana dili hilo na United, ambalo litashuhudiwa miamba hiyo ya soka kutoka Serie A ikitoa kitita cha paundi milioni 13.5 kwa ajili ya Sanchez.
Inadaiwa sehemu ya makubaliano hayo ni kuwa nyota huyo atatangazwa rasmi baada ya mchezo wao dhidi ya Getafe wa michuano ya Europa League siku ya Jumatano.
Inter inamsajili Sanchez kwa dau la paundi milioni 13.5 kwa mkataba wa miaka mitatu ambapo atasalia hapo hadi mwezi Juni mwaka 2023.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 31 alipaswa kurejea United, Agosti 7 ili kwenda kumalizia miaka yake miwili lakini sasa atasalia hapo.
Aliibukia ndani ya united msimu wa 2018 akitokea Klabu ya Arsenal alipelekwa Inter Milan kwa mkopo msimu wa 2019.