Home Uncategorized USAJILI WA MBWEMBWE SAWA, MUHIMU WEKEZENI KATIKA MAANDALIZI

USAJILI WA MBWEMBWE SAWA, MUHIMU WEKEZENI KATIKA MAANDALIZI



Na Saleh Ally

HOFU ya ugonjwa wa Covid 19, imebadilisha mambo mengi sana katika mlolongo sahihi wa maisha ya mpira wa soka duniani.

 

 Kwa miaka nendarudi, mambo ya mpangilio ya mchezo wa soka yalikuwa yanajulikana dunia nzima. Yalikuwa yanakwenda kwa utaratibu sahihi ambao unaweza kusema uko fixed.

 

 

Baada ya ligi mbalimbali kusimama, mambo yakaanza kubadilika, baadhi ya nchi zikaanza kwenda mwendo wa kujitegemea na si ule mfumo au mifumo iliyokuwa inajulikana kwa miaka nendarudi.

 

Ndio maana unaona, baadhi ya nchi ziliamua mapema kabisa kusitisha ligi zao ambazo hazikufikia ukingoni na kuamua kutangaza bingwa wao.

 

Baadhi ya nchi zikasema hapana, zitaendelea hadi mwisho. Ligi zikaendelea bila ya kuwa na mashabiki hadi mabingwa walivyopatikana. Hapa nyumbani Tanzania, sisi ligi ikaendelea na mashabiki wakaruhusiwa lakini kukawa na utaratibu mzuri wa mashabiki kuingia uwanjani kwa ajili ya ile sheria ya “Social Distancing”.

 

Nimeanza kukumbushia hiyo kwa kuwa kwa sasa, wachezaji katika Ligi Kuu Bara walipata mapumziko kwa muda mfupi sana na wanatakiwa kuanza kazi mara moja kwa kuwa msimu mpya utaanza Septemba 6, ikiwa ni wiki kadhaa tu baada kumalizika kwa Ligi Kuu Bara na fainali za Kombe la Shirikisho la Azam Sports.

 

Hii ni hali tofauti kidogo na ilivyozoeleka na ndio maana nikasema kuna mambo ya aina mbili ninayoweza kushauri nikianza na upande wa wachezaji na baadaye viongozi.

 

  


Najua timu zitategemea sana usajili mpya kama sehemu ya kujiamini, lakini bado nishauri kwa wachezaji lazima wabadili hisia zao kuondoka katika yale mazoea. Mapumziko yalikuwa mafupi, si kama yale ambayo wameyazoea. Maana yake, ili kufanya vizuri lazima wakubaliane na ile hali kwamba ilikuwa ni lazima ifanyike namna hii.

 

Hivyo, wakae sahihi na kurudi mchezoni kwa kuwekeza akili zao katika maandalizi kwa ajili ya msimu mpya. Kisayansi, mwili wa mwanadamu umeumbwa kuwa na uwezo wa kupambana au kupinga na kimawazo ukiupelekea huko, utapinga hata vilivyo sahihi.

 

SOMA NA HII  SIMBA YAKWEA PIPA KUIFUATA MBEYA

Kama kuna mchezaji ataanza kuamini hakupumzika vya kutosha, baadaye ndio huyo ataanza kutegemea mazoezi, kupumzika sana au hata kusingizia ana matatizo ya kifamilia, jambo ambalo ni la kisaikolojia na vizuri kupambana nalo mapema kuwa hii ndio “hali halisi ya wakati huu”.

 

Kwa upande wa viongozi na hata makocha, pia wanapaswa kujua mambo yamebadilika na maandalizi yanapaswa kuwa tofauti kidogo.

 

 

 

Ule mpangilio wa maandalizi ya mwanzoni mwa kambi, unapaswa kuwa tofauti na inawezekana hata benchi la ufundi lazima libadili ratiba kwa kuwa wakati ule muda ulikuwa mwingi wa mapumziko na wa kutosha wa maandalizi, sasa sivyo.

 

Maana yake, programu ya benchi la ufundi inapaswa kuwa tofauti na ile ya awali kama ilivyozoeleka. Lazima iwe ina ugumu kidogo kutokana na uchache wa muda. Maana yake, mazoezi magumu ya mwanzo kwa ajili ya utimamu wa mwili, kuanza kulainisha na kuingia katika mechi za kirafiki kuwe mfululizo.

 

Pamoja na hivyo, kupanga programu nzuri ya kuingia katika mechi za kirafiki ambazo kwa makocha watalazimika kuziona timu zao kwa ufasaha na kuanza kusuka muunganiko wa kikosi.

 

Hii yote itakwenda katika ule mfumo ambao ni tofauti kidogo na ule ambao unakuwa umezoeleka mara zote.

 

Kwa upande wa viongozi, wanapaswa nao kuhakikisha maandalizi yanakuwa na uhakika kwa maana ya makocha na wachezaji wanapata kila wanachohitaji kwa wakati mwafaka ili kuepusha kuwaudhi kila mara kwa kukosa vitu ambavyo wanaamini wanastahili kuvipata.

 

 

 

Kama wataingia katika maudhi, hata kama wao walijiweka vizuri kisaikolojia, wanaweza kujikuta wametoka relini wakati ndio wanajiandaa kuanza ligi.

 

Iwapo kuna makundi kati ya haya, yatapuuzia kuna hatari ya mambo kutokwenda vizuri kwa kuwa mwenendo wake ni mfumo, unategemeana kutoka katika kundi moja kwenda jingine.

 

 

Kuvuruga upande mmoja tu kupitia mfumo, ni kuvuruga kila kitu na ligi ndio inakwenda kuanza mapema mwezi ujao, timu itakayoanza vibaya kwa kuwa haikujipanga mwanzo, itakuwa na wakati mgumu sana kurejea relini.