Home Uncategorized MAJUKUMU MAPYA YA SENZO WA SIMBA NDANI YA YANGA HAYA HAPA

MAJUKUMU MAPYA YA SENZO WA SIMBA NDANI YA YANGA HAYA HAPA

 


KLABU ya Yanga leo Agosti 24 imemtambulisha rasmi aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa kuwa mshauri wao.

Senzo atashirikiana na uongozi wa klabu na kampuni ya GSM kwenye mazungumzo ya mabadiliko ya mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo wakishirikiana na watu wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) na Klabu ya Sevilla ya Hispania, kuanza mchakato mzima.

 

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla, amemtambulisha Senzo mbele ya wanahabari na kusema kuwa sasa kazi ya kuubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo unaanza rasmi.

 

“Yanga SC tumemchukua Senzo kama mshauri wetu hasa kwenye haya mabadiliko tunayokwenda kuyafanya. Tunao washauri wa La Liga na Sevilla, tumeona na yeye tumuongeze sababu ana rekodi nzuri ya uongozi wa masuala ya soka, na ameshaanza kushiriki vikao vyetu,” amesema.

 

Senzo amesema;“Si kazi rahisi kujiunga na Yanga kwa sababu ni moja ya klabu kongwe, kubwa na yenye historia nzuri barani Afrika. Kwangu ni bahati, nitafanya kazi ya kuishauri klabu na kuhakikisha tunaingia kwenye mfumo mpya, wa kisasa kuiongoza klabu ili kuwa tayari kushindana.

 

“Nitakuwa mshauri na kiunganishi kati ya La Liga na Sevilla pamoja na Yanga, nitatoa ushirikiano wangu wote kwa kushirikiana na viongozi wa klabu pamoja na GSM kuleta mafanikio ndani ya klabu, hivyo sasa najisikia mwanafamilia wa Yanga ,” amesema.


Senzo ameibukia Yanga akitokea Simba, Agosti 9 muda mfupi baada ya kutangaza kubwaga manyanga ndani ya Simba.

SOMA NA HII  AZAM FC YATOSHANA NGUVU NA RUVU SHOOTING