REAL Madrid, wameongeza wasiwasi kuhusu uimara wa nyota wao Eden Hazard kutokana na kushindwa kuwa fiti kuitumikia timu yake ya Taifa ya Ubelgiji licha ya kuwa kwenye kikosi cha timu hiyo.
Hakuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kilichoshinda mabao 5-1 mbele ya Iceland, Septemba 8 pamoja na ule walioshinda mabao 2-0 mbele ya Denmark.
Hazard hakuyeyusha hata dakika moja uwanjani na Kocha Mkuu Roberto Martinez amesema kuwa hakuwa katika ubora wa kutosha kuanza kwenye mechi hizo ambazo zilikuwa na ushindani mkubwa.
Ripoti zinaeleza kuwa Real Madrid wanazidi kuchanganyikiwa wanaposkia kwamba uzito wa nyota huyo umepitiliza kiwango jambo linalowafanya wafikirie mbadala wake kwa ajili ya msimu mpya wa 2020/21.
Kwa mujibu wa Diario Sport imeeleza kuwa Hazard ambaye aliibukia ndani ya Real Madrid kwa dili la pauni milioni 150 msimu wa 2019 imeeleza kuwa bado kuna mashaka kwamba kama nyota huyo anaweza kudumu ndani ya kikosi hicho kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara pamoja na suala la uzito kuwa juu.
Hazard mwenye miaka 29 ana kazi ya kufanya ili kuweza kurejea kwenye ubora wake kama alivyokuwa ndani ya Chelsea ambapo alicheza jumla ya mechi 245 na alifunga mabao 85.
Mambo yamekuwa magumu ndani ya Real Madrid ambapo amecheza jumla ya mechi 16 na kufunga bao 1.