UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa upo tayari kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Septemba 20, Uwanja wa Sokoine Mbeya dhidi ya Mbeya City.
Mchezo huo utakuwa ni wa kwanza kwa Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba kucheza nje ya Dar kwa kuwa mechi zote mbili ilicheza pale Uwanja wa Azam Complex.
Imecheza mechi mbili na kushinda zote ilianza mbele ya Polisi Tanzania, Septemba 7 kwa ushindi wa bao 1-0 kisha ilishinda mabao 2-0 mbele ya Coastal Union.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa kwa sasa wachezaji wote wapo tayari kwa ushindani na lengo ni kufikia malengo ambayo wamejiwekea.
“Tunaamini kwamba kuanza kwa ushindi kwenye mechi zetu za awali ni mwanzo mzuri, tunatambua kwamba kuna mechi nyingine ngumu ila tutapambana kupata matokeo chanya,” amesema.
Mbeya City itakuwa nyumbani ila kwa mara ya kwanza baada ya kuyeyusha pointi sita ugenini ilianza kupokea kichapo cha mabao 4-0 mbele ya KMC kisha ikapoteza kwa kufungwa bao 1-0 mbele ya Yanga.