Kagera Sugar itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kuyeyusha jumla ya pointi tano kati ya sita ambazo walikuwa wanazisaka kwenye mechi mbili ambazo wamecheza.
Ilianza kupokea kichapo cha bao 1-0 mbele ya JKT Tanzania Uwanja wa Kaitaba, Septemba 7 kisha ikaambulia sare ya bila kufungana mbele ya Gwambina FC, Uwanja wa Gwambina Septemba 11, inakutana na Yanga iliyotoka kushinda bao 1-0 mbele ya Mbeya City.
Akizungumza na Saleh Jembe, Maxime amesema kuwa wamejipanga kwa ajili ya mchezo kwa ajili ya mchezo huo wanahitaji pointi tatu ili kurejesha makali yao ndani ya ligi.
“Mechi mbili za mwanzo kwetu hazikuwa rafiki hasa kutokana na kushindwa kupata matokeo mazuri, kwa sasa tupo nyumbani na tunatambua kwamba tutacheza na Yanga, tunawaheshimu wapinzani wetu lakini lazima tupambane kupata pointi tatu muhimu,” amesema Maxime.
Mchezo wa mwisho uliowakutanisha Kagera Sugar na Yanga, Uwanja wa Kaitaba msimu uliopita, Yanga ilishinda bao 1-0 hivyo Kagera Sugar itapambana kuvunja rekodi yao ya msimu uliopita.