MKURUGENZI wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said amesema kuwa matokeo chanya ambayo wanayapata Yanga kwa sasa kwenye mechi zao tatu zilizopita yanawapa matumaini ya kuendelea kufanya vizuri.
Yanga ikiwa imecheza mechi tatu za ligi, imeshinda mechi mbili na kulazimisha sare moja ambapo kibindoni imefunga mabao matatu na kati ya hayo mawili yakifungwa na wachezaji wapya wawili ambao ni Tuisila Kisinda na Michael Sarpong.
Hersi amesema kuwa kwa namna ambavyo wachezaji wanapambana ndani ya uwanja kunawapa matumaini ya kufikia malengo yao waliyojiwekea.
“Ni faraja kubwa kuanza kupata matokeo baada ya kile ambacho tulitarajia kukifanya msimu huu. Timu yetu tuliijenga na tuliangalia kufanya makubwa kwenye kila idara ikiwa ni kuifanya timu irudi kwenye ubora.
“Tunachotaka ni kuendelea kupambana zaidi kwa ajili ya kufanikisha ndoto za kuwa mabingwa kwa msimu huu na bado tunaona kikosi hakijawa sawa kikiwa kamili zaidi kwa maana wakijuana basi tutakuwa na uwezo wa kufanya makubwa kuliko ilivyo kwa sasa,” alimaliza Hersi.
Mchezo wa Yanga unaofuata Septemba 27 kitamenyana na Mtibwa Sugar, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.