UONGOZI wa Yanga umesema kuwa kwa sasa hauwezi kuzungumzia ishu ya kuitaka saini ya nyota namba moja ndani ya Simba, Clatous Chama.
Chama amekuwa akitajwa kuondoka ndani ya Simba huku habari zikieleza kuwa miongoni mwa timu ambazo zinaitazama saini yake kwa ukaribu ni pamoja na Klabu ya Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Zlatko Krompotic.
Akizungumza na Saleh Jembe, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema kuwa hawezi kuzungumzia suala la Chama kwa kuwa hajui chochote kuhusu suala hilo.
“Kuhusu Chama kiukweli siwezi kulizungumzia kwa sasa nisije nikawa muongo, sijui chochote kuhusu Chama ila ninachojua mimi tuna kikosi kizuri ambacho kinashindana ndani ya ligi na nina imani tutafanya vizuri,” amesema Mwakalebela.
Chama mkataba wake ndani ya Simba unameguka Julai 21 ambapo akiwa ndani ya Simba msimu uliopita aliweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora na kiungo bora kwa msimu wa 2019/20.