SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa taarifa kwamba kimetokea malalamiko ya Klabu ya Yanga kuhusu uhalali wa mkataba kati ya mchezaji Bernard Morrison na Simba.
Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo imeeleza kuwa malalamiko hayo yanafanyiwa kazi.
Jana, Oktoba Mosi, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela aliweka wazi madai kuwa wamebaini mapungufu makubwa kwenye mkataba wa Morrison jambo ambalo wanahitaji haki itendeke.
Mwakalebelea alibainisha kuwa miongoni mwa mapungufu yalikuwa kwenye mkataba huo ni kutokuwepo kwa saini ya upande wa Simba pamoja na mashahidi jambo linalofanya mkataba huo uwe batili.
Morrison alikuwa mchezaji wa Yanga kwa msimu wa 2019/20 ambapo aliondoka ndani ya klabu hiyo kwa mvutano mkubwa kutokana na Yanga kudai kwamba ana mkataba wa miaka miwili huku yeye akieleza kuwa ana mkataba wa miezi sita.