BAADA ya Biashara United ya mkoani Mara kupata sare ya kutofungana na timu ya Ruvu Shooting, Kocha Mkuu wa timu hiyo Francis Baraza amesema timu yake imejipanga vilivyo kuhakikisha inapata matokeo katika mchezo wake na Mtibwa Sugar ambao utachezwa leo Oktoba 4.
Baraza amesema“ Baada ya kucheza michezo miwili ugenini na kuambulia pointi moja, kiukweli tumejipanga kuona tunafanya vizuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani kwa kuwafunga Mtibwa.
“Najua utakuwa mchezo mgumu kwa timu zote kwakuwa kila timu inao ubora wake lakini sisi Biashara tumejipanga kufanya vizuri zaidi.
“ Malengo yetu ni kuona tunapata matokeo katika kila mchezo ambao tunacheza kwenye uwanja wa nyumbani maana ligi ya msimu huu ni yatofauti sana na tunatakiwa kukusanya pointi mapema ili mwisho wa siku tusiwe katika ile presha ya kushuka daraja.
“Kama benchi la ufundi tumefanyia kazi mapungufu ambayo tuliyaona tangu mchezo wa Simba na mchezo wa Ruvu Shooting na kikubwa tumeyafanyia kazi na kiukweli wachezaji wanaonekana kubadilika na matarajio yetu ni kupata matokoe kwenye mchezo wetu ambao utachezwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza,” amesema.
Mtibwa Sugar wao wametoka kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 na Yanga leo wanakutana na Biashara United iliyotoka kulazimisha sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting na mchezo wake wa raundi ya tatu ilifungwa mabao 4-0 na Simba.