MZUNGUKO wa sita upo njiani ambapo kuna mchezo uliopaswa kuchezwa Oktoba 18 kati ya Yanga na Simba ulipelekwa mbele na sasa utachezwa Novemba 7.
Licha ya mchezo huo kupelekwa mbele kuna mechi za mzunguko wa sita zinawahusu Yanga na Simba tena wanacheza bila mashaka.
Oktoba 22 ni Tanzania Prisons dhidi ya Simba mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Nelson Mandela na Oktoba 22 Yanga dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Mkapa.
Kwa harakahara hapa unaweza kuona ni namna gani vikosi vyote viwili vitaingia uwanjani kusaka pointi tatu muhimu kwenye mechi za Ligi Kuu Bara.
Tatizo linakuja kwamba wachezaji wote bado hawajarudi na angalizo ambalo lilikuwa limetolewa awali na Bodi ya Ligi Tanzania,(TPLB) ni kwamba wachezaji ambao wameitwa kwenye timu zao za taifa wanaweza kuathiri vikosi hivi viwili.
Ninaona kwamba kuna mambo hapa yanaendelea huku maswali yakiwa mengi lakini kama ni hivyo basi inabidi tuwekwe wazi kwamba kuna mechi maalumu na nyingine ni za kawaida.
Ikiwa wachezaji ambao walishindwa kucheza mechi za ligi Oktoba 18 sababu ikiwa ni kurejea kwao kuwa tatizo na vikwazo vya usafiri hesabu zipi zimetumika kumaliza vikwazo ndani ya siku nne?
Ukweli ni kwamba tuna safari ndefu kufikia mafanikio kwenye soka letu kwa sasa kutokana na mwenendo wake ulivyo kikubwa ambacho kinatakiwa kuwekwa sawa kwa sasa ni usawa kwa mechi zote.
Msimu uliopita mambo yalikuwa safi panguapangua zilikuwa hazina kasi kubwa ila msimu huu mambo yameanza mapema sasa kasi hii inabidi itafutiwe dawa.
Miongoni mwa vinavyopoteza ladha kwenye soka letu la Bongo ni pamoja na panguapangua ya ratiba yetu hivyo kwa wakati ujao ni muhimu kutazama namna gani mwendo utakuwa sawa bila kuweka mazingira ya kuwaumiza wengine.