UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa hesabu zao kubwa ni kuona wanatimiza mipango yao kwanza waliyojiweka huku wakiziweka kando Simba na Yanga.
Kwa sasa Azam FC ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi tano huku Simba ikiwa nafasi ya pili na Yanga ipo nafasi ya tatu, zote zina pointi 13.
Tofauti yao ni kwenye idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ambapo Simba imefunga mabao 14 na kufungwa mabao mawili huku Yanga ikiwa imefungwa bao moja na kufunga mabao saba.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa mpango namba moja kwa Azam FC ni kutimiza malengo waliyojiwekea jambo litakalowafanya wazidi kuwa washindani.
“Tumejifunza kupitia makosa na wakati uliopita ulikuwa ni darasa tosha kwetu kwa sasa tunapambana kuona namna gani tunaweza kufikia malengo yetu kabla ya kuwafikiria wengine.
“Kuanzia kwa wachezaji, benchi la ufundi nao pia wanatambua kwamba kuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya kabla ya kufikia malengo ambayo tumejiwekea.
“Bado ligi ni mbichi lakini tunamshukuru Mungu kwa kuwa mechi zetu za mwanzo tumepata matokeo nasi tunahitaji kuendelea kupata matokeo chanya,” amesema.
Oktoba 15, Azam FC itawakaribisha Mwadui FC kwenye mchezo wa ligi utakaochezwa majira ya saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex.