CEDRIC Kaze Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa, ana matumaini makubwa ya kuuchukua ubingwa kutokana na mipango yake makini pamoja na uimara wa kikosi chake.
Kaze amesaini dili la miaka miwili kukitumikia kikosi cha Yanga akichukua mikoba ya Zlatko Krmpotic ambaye alifutwa kazi Oktoba 3, tayari amesahaanza kazi rasmi kukinoa kikosi chake kipya.
Kwa sasa Yanga ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza mechi tano na vinara ni Azam FC wenye pointi 18 wakiwa wamecheza mechi sita.
Kocha huyo raia wa Burundi amesema kuwa hana hofu kwa kuwa wameachwa kwa pointi tano na bado wana mchezo mkononi hivyo wakishinda watabakiza pointi mbili kuwafikia vinara wa ligi.
“Mimi siwezi kufanya maandalizi ya kikosi changu kwa kwa ajili ya Simba pekee na badala yake ninafanya maandalizi kwa kila timu nitakayokutana nayo katika michezo inayofuatia ya ligi.
“Hivyo kila mchezo kwangu ni fainali na tutapambana kama fainali bila ya kuidharau timu yoyote, kikubwa mashabiki waondoe hofu kwenye mbio za ubingwa ligi, licha ya Azam kuwepo kileleni wakituongoza ambao nao wapo mbele kwa mchezo mmoja.
“Malengo yangu niliyokuja nayo ni kuipa ubingwa ambayo nimepanga kuyatimiza katika msimu huu, uzuri ninawafahamu na kuwafuatilia wachezaji wote tangu nikiwa Canada nilikuwa nikiwasiliana na kocha msaidizi Mwambusi (Juma) nikimpa program za mazoezi.
“Niwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa ndani ya muda mfupi nikiwa na kikosi changu wataona mabadiliko makubwa ikiwemo timu kucheza soka safi la kuvutia na kuelewana.
Mchezo wa Yanga unaofuata ni dhidi ya Polisi Tanzania Oktoba 22, Uwanja wa Mkapa utachezwa saa 1:00 usiku.