NYOTA wa Simba, Bernard Morrison huenda ataukosa mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaoihusu timu yake ya zamani ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Novemba 7, Uwanja wa Uhuru.
Morrison mwenye pasi moja ya bao kati ya 14 yaliyofungwa na Simba kwa msimu wa 2020/21, alionekana akimpiga ngumi mchezaji wa Ruvu Shooting, Juma Nyosso kwenye mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Uhuru wakati timu yake ikichapwa bao 1-0.
Tukio hilo lilitokea baada ya mpira kusimama dakika ya 72, kutokana na wachezaji wa timu zote mbili kuwa kwenye mzozo uliotokana na mwamuzi kuamua Simba ipige penalti baada ya mchezaji Luis Miquissone kuonekana akichezewa faulo ndani ya 18.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 39,(21) kanuni za Ligi Kuu, Toleo la 2020, kuhusu udhibiti wa wachezaji inasema kuwa mchezaji yeyote atakayethibitika na kupatikana na hatia ya kumpiga mchezaji mwenzake isivyokuwa kawaida au kwa kutumia nguvu kubwa kuliko kawaida/kupigana ama kumpiga mwamuzi, kijana wa mpira, au ofisa, mhudumu mwingine wa mchezo atasimama kushiriki michezo isiyopungua mitano (5).
Kanuni hiyo inaeleza kuwa anaweza kufungiwa kati ya miezi mitatu mpaka mwaka mmoja na faini isiyopungua 1mil bila kujali hatua iliyochukuliwa na mwamuzi uwanjani na kwa mazingatio ya kanuni ya 39:5.3.
Hivyo ikiwa Kamati ya Maamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania itatoa hukumu yake hivi karibuni ni wazi kuwa katika michezo mitano ambayo Morrison ataikosa ni pamoja na ule dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Novemba 7.
Kama adhabu hiyo itatolewa kabla ya Simba hawajacheza mchezo wowote kuanzia sasa inamaana kuwa atakosa mchezo dhidi ya Mwadui, Kagera Sugar, Yanga, Dodoma Jiji na Polisi Tanzania.
Hata hivyo, anaweza kufungiwa zaidi ya hiyo au michache.Pamoja na kwamba mwamuzi hakuliona tukio hilo, lakini ni dhahiri kuwa kutokana na ukuaji wa teknolojia wa sasa, kamati hiyo inaruhusiwa kuangalia marudio ya mchezo huo na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria.