Home Uncategorized CHONDE, CHONDE, RANGI ISIWE KISINGIZIO CHA KUJENGA CHUKI, UADUI KATIKA VIWANJA VYA...

CHONDE, CHONDE, RANGI ISIWE KISINGIZIO CHA KUJENGA CHUKI, UADUI KATIKA VIWANJA VYA SOKA…

Na Saleh Ally

UMEWAHI kusikia mashabiki wa Manchester United, Manchester City, Real Madrid, Barcelona, Juventus wamepigana kwa ajili ya rangi? Najua utanijibu hapana.

Hapa nazungumzia mashabiki wa timu kama hizo, za kariba ya aina hiyo na mashabiki hasa ambao ni asilia ya timu hizo kwa maana ya wale wanaotokea barani Ulaya.

Mashabiki hawa wanakuwa wanajua timu zao zinahitaji nini, wanaelewa maana ya wao kuwa mashabiki na wanajua kuwa furaha na faraja ndio jambo namba moja kwao.

Utambulisho wa timu, unajulikana na lazima shabiki aelewe kuwa rangi na nembo ni jambo ambalo linahusika katika utambulisho lakini bado hakuna klabu hata moja duniani ina uwezo wa kumiliki rangi zake peke yake.

Kwa rangi haiwezekani, hakuna mmiliki wa rangi lakini zinaweza kutumika katika mambo mengi sana, katika soka moja ni utambulisho.

Nembo inawezekana kila klabu kuwa na nembo yake ambayo inatambulika ikiwa na ujumbe ambao inafikisha kulingana na hali fulani.

Kama nembo kila klabu inaweza kumiliki yake, basi huu ndio utambulisho namba moja wa klabu ambao unapewa nafasi ya kwanza na unapaswa kuheshimiwa.

Msisitizo wangu hapa ni hivi, rangi za njano na kijani zinaitambulisha Yanga, nyekundu na nyeupe zinaitambulisha Simba na unaona, wakati Simba wanatengana na Yanga walichagua rangi tofauti ili watofautiane nao. Lakini tukubali rangi haziwezi kugeuka na kuwa kitu kinachotumika kujenga kutoelewana, kuchukiana hadi wakati mwingine kufikia kuwa uadui.

Tumeona mara nyingi mashabiki wa Yanga na Simba wakifikia hadi kupigana, kuchaniana nguo na jezi, kudhalilishana eti kisa rangi. Swali linakuja, nani hasa mmiliki wa hizo rangi?

Mfano tunaona mtu katika soka ni Simba (rangi nyeupe na nyekundu), katika siasa ni CCM (rangi njano na kijani). Sasa huyu anapaswa kuzichukia rangi hizi kwa sababu ipi?

Wakati mwingine katika soka, mtu anaishangilia Yanga (njano na kijani) lakini anaipenda Arsenal (nyekundu na nyeupe). Na utaona baadhi hadi wanayafinya mapenzi yao kwa madai hawawezi kuvaa jezi nyekundu ya Arsenal wakati Arsenal inaanza kuonekana kwa jezi hiyo nyekundu na nyeupe.

SOMA NA HII  SERIKALI YAFIKIRIA KUREJESHA LIGI ZOTE NCHINI

Kuna vitu vya kujifunza na tukaamua kuachana na ushamba wa rangi. Ushambu huu umewafanya mashabiki wengi kuumizana au kujengeana uadi. Pia tunaweza kupunguza heshima ya kupindukia katika rangi mbalimbali za klabu mnazozipenda na kufanya ni kitu cha kawaida kwa kuwa rangi inayotumika Yanga au Simba leo, kesho utaikuta inatumika katika kitu kingine kabisa ambacho huenda hakikuvutii hata kidogo.

Klabu zenu hazimiliki rangi hata moja, ila zinatumia rangi ambazo pia zinaweza kutumiwa na klabu nyingine au jambo jingine kwa kuwa ndio dunia ilivyo na hili haliwezi kubadilika.

Kuendelea kuumizana na kudhalilishana kisa eti huyu kavaa rangi fulani ni kuonyesha kutojitambua katika kiwango kilichopitiliza.

Watu wanaumizwa na ajabu watu wanafurahia, jambo hili si sahihi kwa maana ya uvunjifu wa kisheria na ukiukwaji wa haki za binadamu. Mambo haya yote mawili hayakubaliki katika mchezo wa soka kwa kuwa ni mchezo wa kistaarabu.

Anayekwenda mpirani na kutaka kuumiza wenzake, maana yake si mpenda soka wala mwanamichezo. Hawezi akawa na nia nzuri au njema na mchezo huo badala yake ni yale matakwa ya kupenda sifa zisizo na msingi lakini akiwa anavunja sheria za nchi na kukiuka haki za kibinadamu.

Nakukumbusha, usidhani unaweza kuwaonea watu kila siku. Kuendelea kufanya uovu ni kutengeneza chuki ambayo ni mbaya sana kwa kuwa ina katika mioyo ya unaowaonea, kuna siku wakisimama na kuamua kulipiza itakuwa shida. Hivyo, si sahihi kupiga au kuwadhalilisha watu kwa kisingizio cha rangi. Soka bado inabaki kuwa sehemu ya upendo na umoja.

Mpira una faida nyingi, moja kubwa ni kuwaunganisha watu hata waliokuwa wametengana hivyo, si sahihi hata kidogo suala la vurugu kupitia jazba za kutunga kwa visingizio vya rangi. Tubadilike.