BEKI wa Klabu ya Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Trent Alexander-Arnold ameongezeka kwenye idadi ya wachezaji majeruhi ambao watakosekana ndani ya uwanja kwa kuwa yeye imeelezwa kuwa atakuwa nje kwa muda wa mwezi mmoja.
Beki huyo aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu England Uwanja wa Etihad kwenye sare ya kufungana bao 1-1 na kwenye wiki nne hizo ambazo atakuwa nje ya uwanja hatashiriki pia kwenye kazi ya timu ya Taifa ya England.
Jurgen Klopp, Kocha Mkuu wa Liverpool amesema kuwa nyota huyo hatakuwa ndani ya uwanja mpaka pale atakapokuwa fiti ambapo kwenye Ligi Kuu England anatarajiwa kukosa mechi kati ya Leicester, Brighton na Wolves, pia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya itakayochezwa Uwanja wa Anfield dhidi ya Atalanta na Ajax.
Liverpool itacheza mechi hizo pia bila uwepo wa beki wake kisiki Virgil van Dijk ambaye naye ni majeruhi na atakuwa nje kwa muda wa msimu mzima pamoja na Fabinho ambaye anatarajiwa kurejea uwanjani baada ya mapumziko yaliyotolewa kutokana na timu za taifa kuwa kazini
Pia kiungo Thiago Alcantara ambaye amecheza dakika 135 baada ya usajili wake akitokea Klabu ya Bayern Munich kwa dau la Euro milioni 20 bado anapewa matibabu baada ya kupata changamoto kutoka kwa Richarlison wakati wa Merseyside Derby Oktoba 17.