CLATOUS Chama, kiungo mtengeneza mipango namba moja ndani ya Klabu ya Simba inaripotiwa kwamba msimu ujao anaweza akasepa ndani ya kikosi hicho kutokana na timu nyingi kuweka ofa mezani wakihitaji huduma yake.
Ndani ya Simba ambao ni mabingwa watetezi na kwa sasa wana kibarua cha kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa ikiwa imefunga jumla ya mabao 22 yeye amehusika kwenye jumla ya mabao saba akifunga mawili na kutoa pasi tano.
Miongoni mwa timu ambayo inapewa kipaumbele cha kupata saini yake ni pamoja na watani zao wa jadi Yanga ambao wao wanahitaji kulipa kisasi cha watani zao hao wa jadi kuipata saini ya Bernard Morrison.
Awali Yanga kupitia kwa Mjumbe wa Usajili,Injia Hersi Said ambaye anaiwakilisha Kampuni a GSM wadhamini wa Yanga alisema kuwa hakuna mpango wa kupata saini ya mchezaji wa Simba ila ikitokea pendekezo la mwalimu na wakafikia makubaliano basi kila kitu kitawekwa wazi.
“Hakuna mpango wa kumchukua mchezaji kutoka Simba kwa sasa lakini ikitokea pendekezo la mwalimu nina amini tutalifanyia kazi.
“Tuliwahi kuzungumza na wakala wa mchezaji Chama (Clatous) akatuambia ana mkataba hivyo hatukuwa na chaguo la kufanya hasa ukizingatia kwamba tunaheshimu masuala ya mkataba,” alisema.
Pia Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck aliweka wazi kuwa kwa namna mchezaji wake Chama anavyofanya anaona ni ngumu kwa msimu ujao kuweza kubaki ndani ya kikosi hicho.
“Chama ni mchezaji mzuri ana uwezo mkubwa na ninamkubali lakini kwa namna anavyofanya ndani ya uwanja inaweza kuwa ngumu kwa mchezaji huyu kubaki msimu ujao ndani ya kikosi.
“Kwa kuwa yeye ana maamuzi na anajua anachokihitaji basi ataamua nini afanye na anahitaji nini hasa ukizingatia kwamba mpira ni biashara,”.
Chama kuhusu kujiunga na Yanga aliweka hadharani kwamba ikiwa itatokea ni dili kubwa atasaini mpaka pale mkataba wake utakapokwisha.
“Kuhusu Yanga ama Simba zote ni timu kubwa, ninaweza kusaini popote lakini kwa sasa ni mali ya Simba mpaka mkataba utakapoisha ndipo ninaweza kuweka wazi,’ .