LICHA ya mabosi wa Simba kuweka wazi kwamba kiungo bora ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2019/20 Clatous Chama ni mali yao mpaka msimu wa 2022, Yanga wameweka wazi kwamba muda utazungumza.
Chama ambaye msimu uliopita alisepa na tuzo tatu, ikiwa ni pamoja na ile ya kiungo bora, mchezaji bora pamoja na kuwa ndani ya kikosi bora cha msimu wa 2019/20 anatajwa kuingia kwenye rada za Yanga kwa kile kinachoelezwa kuwa mkataba wake unameguka msimu ujao.
Kiungo huyo ambaye msimu uliopita alihusika kwenye mabao 12 kati ya 78 yaliyofungwa na Simba baada ya kutoa pasi 10 na kufunga mabao mawili, msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa pasi tano za mabao anatajwa kuwa kwenye hesabu za Yanga.
Uongozi wa Yanga kupitia kwa Injinia Hersi Said ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji ndani ya Kampuni ya GSM ambao ni wadhamini wa Klabu ya Yanga aliweka wazi kwamba wanatambua uwezo wa Chama na wanaheshimu mkataba wake.
Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa kuhusu ishu ya nyota Chama licha ya Simba kuweka wazi kwamba ni mali yao muda utazungumza.
“Muda utaongea kwa kuwa wao wameweka wazi kwamba ana mkataba kwa sasa hatuwezi kusema jambo lolote lakini muda utaongea,” alisema Nugaz.