IMEELEZWA kuwa mabosi wa Yanga wamekumbushia dili lao la kumpata kiungo mshambuliaji mzawa, Gerald Mdamu ambaye kwa sasa anakipiga ndani ya Klabu ya Biashara United.
Mdamu aliwekwa kwenye hesabu za Yanga msimu uliopita wakati akicheza ndani ya Mwadui FC ila dili hilo lilibuma baada ya Yanga kupata saini ya viungo wawili Tuisila Kisinda na Tonombe Mukoko kutoka AS Vita ya Congo na wote wamekuwa na uhakika wa namba ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Cedric Kaze.
Habari zinaeleza kuwa mpango wa kumuibua Mdamu ambaye msimu wa 2019/20 aliweka rekodi ya kuwa mtibua mipango namba moja kwa Simba iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems kwa kumfunga kwa kichwa Aishi Manula na kuifanya timu hiyo kuyeyusha pointi tatu kwa mara ya kwanza bado yupo kwenye mafaili ya Yanga.
Mdamu kwa msimu wa 2019/20 aliweza kung’ara ndani ya Mwadui iliyokuwa ipo kwenye hatari ya kushuka daraja aliweza kuwa mhimili wa kikosi hicho ambacho kipo chini ya Khalid Adam na kilijinasua kutoka kushuka daraja.
Akizungumza na Saleh Jembe, Mdamu amesema kuwa kwa sasa yupo zake Biashara United baada ya mambo yake ya kuibukia ndani ya timu kubwa kukwama.
“Kuna timu ambazo meneja wangu alikuwa anafanya nazo mazungumzo zilikuwa ndani ya tano bora msimu uliopita ila kwa kuwa muda ulikuwa mdogo na wengine walikuwa wameshafanya usajili ikanibidi nijiunge na Biashara United ila bado muda upo wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi,” .
Msimu huu wa 2020/21 akiwa ndani ya Biashara United iliyo nafasi ya 4 ikiwa imefunga mabao 6 pasi mbili za mabao ametoa moja alimpa kinara wa utupiaji ndani ya timu hiyo Kelvin Friday wakati wakishinda bao 1-0 dhidi ya mabosi wake wa zamani, Mwadui FC.