BEKI kisiki wa Yanga, Lamine Moro yupo fiti kwa sasa kutokana na majeraha yake ya goti kuwa sawa na ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya kurejea kwenye ubora wake.
Moro aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara, Uwanja wa Mkapa kwenye Dar, Dabi dhidi ya Simba iliyochezwa Novemba 7.
Mchezo huo uliokamilika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Moro aliumia goti baada ya kugongana na beki wa kulia, Shomari Kapombe chaguo namba moja kwa Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck
Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kuwa kwa sasa mchezaji huyo yupo sawa hivyo mashabiki wa timu hiyo wasiwe na mashaka.
“Kwa sasa Lamine Moro hali yake inaendelea vizuri kwa kuwa alifanyiwa vipimo na kupatiwa matibabu ili kuweza kuwa kwenye ubora wake.
“Hakuumia sana kwa kuwa ilikuwa ni mgongano tu ndani ya uwanja hasa ukizingatia kwamba mchezaji wakati mwingine anatumia nguvu na akili nyingi ndani ya uwanja,” amesema.
Yanga ikiwa imefunga mabao 12, Moro amefunga mabao mawili licha ya kuwa ni beki akiwa ni kinara kwa mabeki wenye mabao mengi.
Pia safu ya ulinzi ya Yanga imeruhusu mabao matatu ndani ya ligi baada ya kucheza mechi 10 ambayo ni machache kuliko timu nyingine.
Mwadui FC ni vinara kwa timu ambazo zimefungwa mabao mengi ikiwa imefungwa mabao 20.