TIMU ya Namungo FC imeweka kambi Zanzibar kwa ajili ya kujiwinda na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo itacheza dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan Kusini.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Novemba 28, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar, saa 10:00 jioni.
Awali Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilitoa taarifa kuwa timu hiyo itacheza kati ya Novemba 27 hadi 29 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu amesema kwa sasa kikosi kimeweka kambi Zanzibar ili kujiandaa na mchezo huo.
“Kwa sasa timu ipo visiwani Zanzibar kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki ili tujiweke fiti kuelekea kwenye mchezo huo uliopo mbele yetu.
“Tarehe rasmi ambayo tumechagua ni Novemba 28. Lakini wapinzani wetu tumejaribu kuwafuatilia kwa karibu kutokana na michezo ya kirafiki ambayo wamecheza hivi karibuni ili tuweze kujua aina ya uchezaji wao na naamini kabla ya mchezo tutakuwa tumepata kitu,” amesema.
Namungo na Simba ndiyo timu za Tanzania Bara ambazo zitaliwakilisha taifa kwenye michuano ya kimataifa mwaka huu.
Kabla ya kuvaana na timu ya Sudan Kusini, Namungo itavaana na Yanga, Novemba 22 Uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku.
Itashuka uwanjani ikiwa na kocha mpya Hemed Morocco ambaye amerithi mikoba ya Hitimana Thiery ambaye amefutwa kazi Novemba 18.