CEDRIC Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa anatambua ubora wa wapinzani wake Namungo ambao atakutana nao leo Novemba 22, Uwanja wa Mkapa jambo ambalo limemfanya atafute mbinu ya kupata matokeo kwenye mchezo huo.
Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi 24 inakutana na Namungo FC iliyo nafasi ya tisa na pointi 14 zote zikiwa zimecheza mechi 10 ndani ya ligi kwa msimu wa 2020/21.
Kaze mwenye tuzo ya kocha bora kwa mwezi Oktoba anakutana na Namungo ambayo msimu uliopita chini ya kocha Hitimana Thiery kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa waligawana pointi mojamoja baada ya sare ya kufungana mabao 2-2.
Kaze amesema kuwa wapinzani wake wapo vizuri licha ya kutokuwa na mwendo unaofurahisha kwa upande wao.
“Ukizungumzia Namungo ni moja ya timu ambayo inafanya vizuri, niliona kwa msimu uliopita namna ilivyokuwa kwenye ubora, ila kwa sasa naona mambo yamekuwa tofauti lakini haina maana kwamba haipo vizuri.
“Tutaingia ndani ya uwanja kusaka pointi tatu na nimewaambia wachezaji kwamba wanatakiwa kuwaheshimu wapinzani wetu kwani ni timu nzuri,” amesema Kaze.
Leo utakuwa ni mchezo wa pili Uwanja wa Mkapa kuwakutanisha Yanga na Namungo huku kila timu ikiwa na kocha mpya kwenye benchi la ufundi.
Namungo ilimfuta kazini Hitimana Thiery Novemba 18 sasa yupo Kocha Mkuu Hemed Morroco na kaze alipokea mikoba ya Zlatko Krmpotic aliyefutwa kazi Oktoba 3.