LICHA ya Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Plateau United, lakini Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, amelitaka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kupitia upya vigezo vilivyotumika kuruhusu mchezo wao huo kuchezwa kwenye Dimba la New Jos, Nigeria
wakati uwanja huo haujakidhi viwango vinavyohitajika.
Wikiendi iliyopita, Simba ikiwa ugenini, iliibuka na ushindi huo katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wikiendi hii jijini Dar.
Barbara alisema kwenye kanuni na taratibu za CAF zinaelekeza aina gani ya uwanja unaotakiwa kupewa leseni ya kuchezewa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kama vile ubao wa
kieletroniki kwa ajili ya kuonyesha matokeo, dakika na vitu vingine muhimu ambavyo Uwanja wa Jos hauna.
Akiuzungumzia uwanja huo, Barbara alisema: “Kuna mapungufu mengi sana ambayo uwanja wa Jos unafanya ukose sifa ya kupewa leseni
ya kutumika katika michezo ya kimataifa. Kanuni za CAF zipo wazi, lazima uwanja uwe
na eneo bora la kuchezea, vyumba vya
kubadilishia nguo, ubao wa ‘electronic’ na vitu
vingine vingi ambavyo uwanja huu wa
umekosa.
“Sasa CAF inabidi waweke wazi na watuambie
ni vigezo gani ambavyo vilitumika hadi
kuruhusu na kutoa kibali kwa Uwanja wa Jos
kutumika kwa michezo ya kimataifa.”
KAULI YA TFF
Naye Mwenyekiti wa Mashindano wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), Ahmed Mgoi ambaye
alikuwa mkuu wa msafara wa Simba
uliokwenda nchini Nigeria, alisema: “Mapungufu
yaliyojitokeza kwenye mchezo huo hayana
nafasi tena, kwa sababu mechi ya kwanza
imekwisha na wameshinda, kikubwa Simba
wajipange kwa ajili ya mchezo ujao ili wafanye
vizuri na kusonga mbele.”
KUREJEA LEO
Meneja wa Simba, Abbas Ally, alisema kikosi
kilianza safari jana Alfajiri kutoka Jos, Nigeria
kupitia Ethiopia na kinatarajia kutua kwenye
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
majira ya saa 10:00 jioni.
“Tunashukuru kwa kuanza vizuri michuano hii
mikubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika, licha
ya matokeo ya ushindi tuliyoyapata nikiri kuwa
haukuwa mchezo rahisi kutokana na ubora wa
wapinzani wetu na hata mazingira ya mchezo,
lakini wachezaji wetu walipambana.