WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Yacouba Songne akicheza dakika 401 bila kufunga, Kocha Mkuu, Cedric Kaze amesema bado mchezaji huyo anahitaji muda ili kujenga hali ya kujiamini.
Mshambuliaji huyo raia wa Burkina Faso mwenye rasta, mara ya mwisho kufunga ilikuwa Oktoba 3, mwaka huu wakati Yanga ikishinda 3-0 dhidi ya Coastal Union.
Ilikuwa zama zile za Kocha Mkuu Zlatko Krmpotic ambaye alifutwa kazi muda mfupi baada ya mchezo huo kukamilika.
Baada ya hapo, katika mechi nane zilizofuata Songne hajafunga bao ambapo ametumia dakika 401 akifanikiwa kutoa asisti mbili kwa Deus Kaseke kwenye mchezo dhidi ya Azam FC na JKT Tanzania.
Jumla Songne ametumia dakika 654 akiwa amecheza mechi 13 kati ya 14 akikosekana mechi moja dhidi ya Namungo ambapo Yanga ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1, Uwanja wa Mkapa.
Kaze amekuwa na maamuzi tofauti juu ya nyota huyo kwa kuweka wazi kwamba anauwezo mkubwa ndani ya uwanja hivyo bado ana imani na uwezo wake kwa kuwa anahitaji muda zaidi wa kucheza ili ajenge hali ya kujiamini.
“Ni suala la muda kwake kuwa imara, kwa sasa anahitaji apewe muda na kujengwa kisaikolojia ili awe bora, ninaamini baada ya muda kila kitu kwake kitakuwa sawa,” amesema.