KIKOSI cha Simba leo kimeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na Meddie Kagere dakika ya 77 kwa mkwaju wa penalti baada ya mwamuzi wa kati Elly Sassi kuamua iwe hivyo.
Penalti hiyo ilionekana kuwa tata kwa kuwa wachezaji wa KMC wakiongozwa na nahodha Juma Kaseje ambaye ni kipa mkongwe ndani ya Bongo walionekana wakimlalamikia mwamuzi huyo.
Kagere alipachika bao lake la tano kwa guu lake la kulia na kuifanya Simba kusepa na pointi tatu muhimu mbele ya wapinzani wao KMC ambao walikuwa kwenye ubora.
Dakika za lala salama, mshambuliaji wa Simba, Chris Mugalu alifunga bao ambalo lilikataliwa na mwamuzi wa kati kwa kile alichodai kwamba mfungaji alikuwa ameotea.
Juma Kaseja, nahodha wa KMC amesema kuwa hawakuwa na chaguo la kufanya kwa kuwa matokeo hayawezi kubadilika ndani ya uwanja hivyo wanapambana kwa ajili ya mechi zijazo.
Kwa upande wa mkongwe ndani ya Simba, Erasto Nyoni amesema kuwa walicheza na timu ambayo inafanya vizuri ndani ya ligi jambo ambalo liliwapa ushindani mkubwa.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha jumla ya pointi 32 ikiwa nyuma ya wapinzani wao Yanga ambao wapo nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 37.
Simba imecheza jumla ya mechi 14 huku Yanga ikiwa imecheza mechi 15. Yanga ipo mbele kwa jumla ya pointi tano.KMC ipo nafasi ya tano na pointi 21.