WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba leo wameanza kwa kukubali kichapo cha bao 1-0 mbele ya FC Platinum kwenye mchezo wa hatua ya kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa wa Zimbabwe.
Kikiwa chini ya Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck kilishuhudia bao la kwanza likifungwa na Perfect Chikwende dakika ya 17 baada ya mabeki kufanya makosa ya kumuacha nyota huyo awapite.
Licha ya jitihada walizofanya Simba kuweka usawa mzani bao hilo kipindi cha pili mambo yalikuwa magumu kwa kuwa hawakufanikiwa.
Bao la Chris Mugalu dakika ya 78 lilitaka kuwarudisha kwenye reli ila mwamuzi alikataa kwa kueleza kuwa mfungaji alikuwa ameotea.
Kupoteza mchezo wa kwanza, Simba ina deni la mabao zaidi ya mawili Uwanja wa Mkapa Januari 5.
Kipa Aishi Manula hakuwa na chaguo la kufanya na kuruhusu nyavu zake kutikiswa kwa mara ya kwanza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mechi mbili mbele ya Plateau United aliweka lango lake salama kwa kukaa bila kufungwa ila leo amekwama.
FC Platinum wameonekana kuwa na spidi na mbinu ndani ya uwanja jambo lililowapa kazi Simba kupata ushindi.