UONGOZI wa Azam FC umesema kuwa kwa sasa mambo yamegeuka ghafla na kuwa magumu kutokana na kupata matokeo mabovu.
Ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Gerge Lwandamini imekwama kuibuka na ushindi kwenye mechi mbili mfululizo zaidi ya kuambulia sare.
Ndani ya dakika 180, ikiwa Uwanja wa Azam Complex ilianza kwa sare ya kufungana mabao 2-2 dhidi ya Namungo FC na matokeo hayo yarijirudia mbele ya Ruvu Shooting inayonolewa na Charles Mkwasa.
Kwenye msimamo awali ilikaa nafasi ya kwanza kwenye raundi saba mfululizo baada ya kujikusanyia pointi 21 kwa kuwa ilishinda mechi zote za mwanzo.
Kwa sasa ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 16, Jumamosi Desemba 26 ina kibarua cha kumenyana na Magereza kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya tatu.
Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema: “Sijui kwa nini timu haipati ushindi, kila kitu ambacho kinatakiwa kupatikana ndani ya Azam kinapatikana.
“Wachezaji wote wanapata stahiki zao mapema na kwa wakati, labda utakuwa ni upepo tu mchafu ndio umetupitia, lakini hatujakata tamaa, tutaendelea kupambana ili mambo yaendelee kuwa mazuri,” .
Safu ya ushambuliaji ya Azam FC imetupia jumla ya mabao 23 na katika hayo mkongwe Agrey Moris ametupia bao moja ilikuwa wakati timu yake ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa Azam Complex.