IMEFAHAMIKA kuwa wachezaji wa Simba ndiyo waliomuondoa kikosini Jonas Mkude sambamba na kusimamishwa kazi kutokana na utovu wake wa nidhamu.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa timu hiyo kupitia kwa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez umsimamishe kiungo huyo ambaye wiki ijayo itamuita kwa ajili ya kutoa utetezi wake kwa utovu wa nidhamu ambao ameufanya.
Taarifa zimeeleza kuwa kabla ya uongozi kumpa barua ya kumsimamisha kazi, baadhi ya wachezaji waandamizi wa timu hiyo walimuwekea kikao na kumtaka abadili mwendo wake.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wachezaji hao walichukua hatua hiyo baada ya kiungo huyo kuchelewa mara tatu mfululizo katika msafara wa mchezo wa Mbeya waliocheza dhidi ya Mbeya City, Nigeria walipokwenda kucheza na Plateau FC na ule wa Zimbabwe ambako walikwenda kukipiga na FC Platinum.
Aliongeza kuwa mara baada ya kikao hicho cha wachezaji kiungo huyo aliahidi kubadilika lakini alirudia kosa kwa kuondoka kambini huku simu yake akizima wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Majimaji FC.
“Wachezaji ndiyo walikuwa wa kwanza kumuondoa kambini sambamba na kumtaka kocha wao Sven (Vandenbroeck) kutomchezesha michezo kumi mfululizo ya ligi na mashindano mengine.
“Hiyo ni baada ya kiungo huyo kushindwa kubadilika, licha ya kumuwekea kikao na kumtaka abadilike, hivyo wachezaji walikubaliana kwa pamoja kambini kwa kumuomba kutomtumia Mkude.
“Hivyo Mkude hautamuona katika michezo kumi hata kama uongozi ukimrudisha katika timu, pia kiungo huyo amechukuliwa posho za michezo kumi ambayo ameicheza ya ligi na mashindano ya kimataifa,” alisema mtoa taarifa.
Chanzo:Championi