KIUNGO Mzawa Said Ndemla amemkosha Kocha Mkuu Sven Vandenbroeck na kusema eneo la kiungo mkabaji limepata mchezaji mbadala kuelekea kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC Platinum.
Eneo hilo kwenye mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na zile za kimataifa lilikuwa chini ya mzawa Jonas Mkude ambaye amesimamishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Hivyo kuna uwezekano wa nyota Ndemla kuanza kwenye mchezo wa marudio Januari 6 dhidi ya FC Platinum ikiwa Sven ataamua kumtumia kwenye nafasi hiyo.
Sven amesema kwenye michezo miwili kuanzia ule wa Azam Sports Federation Cup dhidi ya Majimaji wakishinda mabao 5-0, kisha na ule wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu wakishinda 4-0, Ndemla alifanya kazi kubwa ya kuimarisha safu ya ulinzi na ushambuliaji.
Kocha huyo anaamini kuwa mchezaji huyo atakuwa msaada kwenye kiungo cha ukabaji pindi watakapowavaa Platinum kwa kuwa amekuwa akifanya kazi yake vema bila kufanya makosa ya mara kwa mara.
Raia huyo wa Ubelgiji amesema Ndemla amekuwa na kiwango bora kwa siku za hivi karibuni, kwani amekuwa akitimiza majukumu yake kwa asilimia kubwa hasa kwenye eneo la kukaba na kushambulia kiasi ambacho kinampa wakati mzuri wa kuamua ni namna gani mchezaji huyo acheze kulingana na mahitaji yake.
“Ndemla amekuwa imara sana, anatimiza majukumu yake vema, tulimpa majukumu ya kukaba alifanya vizuri. Hiyo inanipa wakati mzuri sana wa kuandaa timu kuelekea kwenye mchezo wa marudiano, kwa kuwa eneo la kiungo mkabaji yupo mtu anayefanya kazi nzuri pia,” amesema Sven.