MTAMBO wa mabao ndani ya kikosi cha Yanga, Yacouba Songne utakosa mechi zote za Kombe la Mapinduzi kutokana na majeraha ya mbavu aliyonayo.
Ndani ya Yanga inayoongoza Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 18 ikiwa na na pointi 44 amehusika kwenye mabao nane kati ya 29.
Songne amefunga mabao manne na kutoa jumla ya pasi nne ambazo zilileta mabao hayo huku pacha yake na Deus Kaseke ikionekana kuwa bora wawapo pamoja.
Nyota huyo aliumia kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu ambapo Yanga ilishinda mabao 3-0, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Januari 5 ambayo ni kesho mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanatarajiwa kuanza ambapo bingwa mtetezi ni Mtibwa Sugar iliyoshinda kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Yanga itaanza kumenyana na Jamhuri, Uwanja wa Amaan mchezo utakaochezwa majira ya saa 2:15 usiku, visiwani Zanzibar.
Daktari wa Yanga, Sheck Mngazija amesema kuwa nyota huyo amepewa mapumziko ya wiki moja ili kurejea kwenye ubora wake.