MIRAJI Athuman, ‘Sheva’ amezidi kutaka ndani ya kikosi cha Simba kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi baada ya leo kupachika bao lake la tatu wakati Simba ikishinda mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Ushindi wa Simba unaipa nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali wanaungana na Yanga iliyotangulia baada ya jana kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Namungo na inafikisha jumla ya pointi nne huku Simba kiwa na pointi sita.
Kiungo Hassan Dilunga alianza kufunga bao la kwanza dakika ya sita kwa pasi ya Mohamed Hussein baada ya kipa wa Mtibwa Sugar kujichangaya.
Sheva alipachika bao la pili dakika ya 37 kwa pasi ya mshambuliaji Chris Mugalu na kuimalizia kwa kichwa kilichopeleka maumivu kwa Mtibwa Sugar.
Mabao yake mawili Sheva alifunga kwenye mchezo dhidi ya Chipukizi wakati Simba ikishinda kwa mabao 3-1, Uwanja wa Amaan.
Pia kwenye mchezo wa leo nyota wapya wa Simba ambao wanafanyiwa majaribio ikiwa ni pamoja na Ion Nyoni na Bernard Agele ambaye ni beki walikuwa sehemu ya kikosi cha ushindi.
Thadeo Lwanga naye ambaye usajili wake umekamilika kwa dili la miaka miwili alianza kikosi cha kwanza kuonyesha makeke yake.
Mtibwa inabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kupata ushindi siku ya leo kwa kuwa walikuwa imara kwenye ulinzi ila nafasi washambuliaji walizokuwa wanapata walikwama kuzibadili kubwa bao.
Dakika ya 22 Issa Rashidi alipiga shuti ambalo lilishindwa kuleta bao akiwa ndani ya 18 na Ibrahim Hilika dakika ya 25 naye alikosa nafasi ya wazi.
Abalkassim naye pia alikuwa na jitihada katika kusaka ushindi na alifanikiwa kupiga shuti moja ambalo liligonga mwamba.
Mtibwa Sugar ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo wameondolewa jumla.