WATANI wa jadi, Simba ikiwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Seleman Matola na Yanga iliyo chini ya Kocha Mkuu Cedric Kaze wanakutana leo Januari 13, 2021 katika mchezo wa fainali wa Kombe la Mapinduzi huku viingilio vikipanda.
Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Amaan ambapo awali tiketi ziliuzwa kwa Sh 3,000, 5,000 na 10,000 lakini hivi sasa zitauzwa kuanzia Sh 5,000, 10,000 na 15,000 ambapo zitauzwa tiketi 12,000 tu.
Pia fainali hizo zitashuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi ambaye atakuwa mgeni rasmi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Khamis Said amesema kuwa hawataongeza tiketi kutokana na uwezo wa uwanja kuwa mdogo na unaingiza idadi ya mashabiki hao hivyo watakaokosa tiketi watalazimika kubaki nyumbani.
“Watu waepuke kununua tiketi feki, tutaanza kuuza tiketi leo saa 3 asubuhi na milango itafunguliwa saa 7 mchana, uwanja wetu hauchukuwi idadi kubwa ya mashabiki na tunaelewa mechi hii ina mashabiki wengi hivyo wote wafuate utaratibu utakaowekwa.
“Ni fainali za aina yake kufanyika kisiwani hapa na itakuwa na mambo mengi yatakayoonyeshwa kuanzia huo muda ambao mageti yatafunguliwa hadi wakati mechi itakapoanza,” amesema Said.
Kuhusu idadi ya wachezaji kama timu zina mpango wa kuongeza, Said amesema kuwa hilo halitakubalika kama mchezaji hajasajiliwa kwenye mfumo wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ambao idadi ni wachezaji 30.
“Kuna taarifa nimesikia kwamba wachezaji wataongezwa, hilo halitakubalika kama wachezaji hao hawakusajiliwa awali tulipotoa mwaliko, tiketi zimepanda bei baada ya majadiliano na kamati,” amesema.