WAKATI kuna baadhi ya mashabiki wa soka wakimbeza, Meddie Kagere na kumuona eti mzee kwa Deogratius Judika Mafie kwake ni tofauti.
Nyota huyo anayekipiga Biashara United, anasema Kagere ni ‘mtu na nusu’ kwa aina ya uchezaji wake na jinsi anavyomkosha kiasi cha kujaribu kugandamizia baadhi ya ujuzi wa straika huyo wa Simba ili kuweza kutengeneza jina lake kwa sasa ndani ya soka la Tanzania.
Judika aliyeanza kucheza kama kiungo kabla ya kubadilishwa kuwa mshambuliaji ameifungia timu yake mabao manne ya Ligi Kuu na moja katika Kombe la Azam (ASFC) kuonyesha namna gani alivyo moto licha ya kuwa na muda mfupi ndani ya ligi hiyo.
Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti katika mahojiano maalumu, Judika ambaye staili ya uchezaji wake wenye kasi na kujua kujiweka katika nafasi huku akifunga mabao muhimu kwa timu yake umemfanya awe na jina kubwa, amefunguka mambo mengi ikiwamo kumzimia Kagere.
Pia amefichua safari yake nzima katika soka na ndoto alizonazo katika kuhakikisha anafika mbali katika soka. Ebu endelea naye;
KAGERE NI NOMA
Judika anasema hakuna mtu anayempa moyo wa kupambana zaidi uwanjani kama, Meddie Kagere wa Simba kwani ndiye mchezaji anayemkubali na kumuiga vitu vingi.
“Namkubali sana Kagere. Napenda anavyojituma uwanjani.Ni mpambanaji asiyechoka ana analijua sana goli yaani huwa hakati tamaa mpaka afunge.
“Amekuwa kama kioo changu, huwa namfuatilia katika mechi nyingi anazocheza na hivyo inanisaidia kuiga baadhi ya vitu ikiwemo roho yake ya kuipambania timu uwanjani, kwani huyu jamaa ni mtu na nusu na mabeki wa timu pinzani bila shaka wanaijua shughuli yake,” anasema Judika ambaye amepanga msimu huu kumaliza ligi akiwa na mabao 10.