UONGOZI wa Simba umesema kuwa hauna mpango wa kumpa dili Mkurugenzi wa Ufundi wa Gwambina FC, Mwinyi Zahera ndani ya kikosi hicho.
Imekuwa ikielezwa kuwa mabosi wa Simba wapo kwenye mpango wa mwisho wa kumalizana na Zahera ambaye aliwahi kuwa kocha ndani ya Yanga kabla ya kuchimbishwa mwanzoni mwa msimu wa 2019/20.
Kwa sasa Zahera ni mwajiliwa ndani ya Klabu ya Gwambina FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara akiwa ni Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi na alipewa dili la mwaka mmoja.
Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema kuwa hawana mpango wa kumpa kazi Zahera kwa wakati wa sasa.
“Kuhusu huyo Zahera mimi simjui na tayari tumeshatangaza benchi letu la ufundi ikiwa ni pamoja na kocha mkuu na kocha wa makipa, ipo nafasi nyingine ambayo tutaitangaza hivi karibuni,”.
Simba imemtambulisha Milton Nienov raia wa Brazil kuwa kocha wa makipa na Didier Gomes raia wa Ufarasa kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa hatua ya makundi na Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho wakiwa ni mabingwa watetezi.