MSHAMBULIAJI mpya wa klabu ya Simba raia wa Nigeria, Junior Lokosa amefunguka kuwa malengo yake makubwa ya kujiunga na Simba ni kuja kushinda mataji kwenye michuano yote iwe ya ndani au ile ya kimataifa.
Mshambuliaji huyo aliyesajiliwa na kutambulishwa rasmi kuwa mchezaji wa Simba siku ya Jumatatu amesajiliwa kama mchezaji huru baada ya kuachana na klabu ya Esperance ya Tunisia aliyoitumikia msimu uliopita.
Ukiachana na Esperance, Lokosa pia amewahi kukipiga na klabu za Kano Pillars na First Bank za kwao Nigeria.
Akizungumzia malengo yake baada ya kusajiliwa na Simba Lokosa alisema: “Nafurahi kukamilisha usajili wangu ndani ya kikosi cha klabu ya Simba, hii ni heshima kubwa kwangu kwa kuwa Simba ni timu kubwa Afrika.
“Kuhusiana na matarajio nisingependa kusema mengi lakini naahidi kujituma kwa uwezo wangu wote kuhakikisha naisaidia Simba kuwa mabingwa wa Afrika kwa kushinda taji la Ligi ya mabingwa Afrika, lakini pia kushinda taji la Ligi Kuu ya Tanzania.
“Najua mashabiki wa Simba wanatarajia mambo mengi kutoka kwangu, naamini taratibu nitaweza kuwafurahisha kwa kuionyesha kiwango cha juu,”