Home Simba SC ISHU YA LWANGA NA SIMBA IKO HIVI

ISHU YA LWANGA NA SIMBA IKO HIVI


UONGOZI wa Klabu ya Simba umefungukia ishu ya kutokuonekana kwa jina la kiungo wao mkabaji raia wa Uganda, Taddeo Lwanga kwenye orodha iliyopelekwa kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), kwa kusema kuwa mchezaji huyo bado ni mali halali ya klabu ya Simba.

Jina la Lwanga halipo kwenye orodha ya majina yaliyopelekwa (TFF), na Simba kama sehemu ya usajili wao wa dirisha dogo wa wachezaji watakaotumika kwenye mzunguko wa pili wa ligi, hali ambayo ilizua maswali mengi kwa wadau wa soka.

Nyota huyo aliyetambulishwa rasmi na Simba Desemba 2, mwaka jana amepata nafasi ya kuichezea Simba katika michuano ya kombe la Mapinduzi ambapo Simba ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kupoteza fainali mbele ya mabingwa Yanga.  

Akizungumzia sakata hilo Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema: “Yamekuwepo maneno mengi kuhusu mchezaji wetu Taddeo Lwanga kutokana na ukweli kwamba jina lake limekosekana katika orodha iliyoenda TFF.

“Lakini niwatoe hofu kwani Lwanga bado ni mchezaji halali wa Simba na kuhusu kinachoendelea tusubiri siku ya utambulisho wa wachezaji kwenye michuano ya Simba Super Cup na wote tutajua,”

SOMA NA HII  MSUVA ATOA KAULI NZITO, SIMBA, YANGA ZATAJWA