Home Yanga SC KAZE AWATIMUA AKINA MUKOKO KAMBINI

KAZE AWATIMUA AKINA MUKOKO KAMBINI


YANGA wamerudi kazini jana na mchana kuanza maandalizi ya mwendelezo wa ligi, lakini wakati mastaa wake wakirejea kambini baadhi wanakutana na balaa jipya wakirudishwa nyumbani kwa muda.

Iko hivi, Kocha Cedrick Kaze aliwapa mapumziko ya siku 10 wachezaji wake kwa sharti moja tu, kwamba wanatakiwa kurejea kambini jana. Yaani saa 6:30 ndani ya alama walitakiwa kuwa ndani ya geti la kambi yao iliyopo kule Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati wachezaji wakiwasili baadhi ya mastaa wakakutana na balaa hilo wakizuiwa kuingia kambini baada ya kufika dakika tano baada ya muda uliopangwa.

“Wamerudishwa, unajua kocha hataki masihara na muda hajali jina lako na wameambiwa warudi walikotoka mpaka atakapowasiliana na viongozi,” kilisema chanzo chetu ndani ya Yanga ingawa jana viongozi walikuwa wagumu kufafanua nini kilitokea na hatma ya mastaa hao.

“Hii ni hatua nzuri kocha anataka kuwaondoa kujisahau baada ya kuchukua kombe, wengine wangeona kama wamemaliza kazi, lakini kumbe bado kuna vita kubwa mbele ingawa baadhi wanadai walichelewa kutokana na msongamano wa pale Kivukoni.”

Mapema juzi, meneja wa Yanga Hafidh Saleh akielezea juu ya ratiba ya kuanza kwao kambi hiyo, alisema hataki kujua mchezaji alikwenda wapi katika mapumziko ya siku 10 walizopewa anachotaka ni saa 6:30 mchana kila mchezaji ambaye alitakiwa kuwasili kambini kuwa humo.

Kaze amekuwa muumini mkubwa wa nidhamu ndani ya kambi ya Yanga ambapo kila kitu anataka kiende na muda kuanzia kula, mazoezi, kupumzika pamoja na mambo mengine.

Yanga imerejea mazoezini kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la FA huku wakishikilia rekodi ya kutopoteza mchezo mpaka sasa ambapo hivi karibuni walitwaa Kombe la Mapinduzi kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Simba.

SOMA NA HII  KAZI INAENDELEA, NCHIMBI , MAYELE WAANZA KUCHEKA NA NYAVU